Soko la madini kufunguliwa KIA

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula wakifungua soko la madini Chunya juzi ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kutaka maeneo yote yenye madini kufungua masoko hayo. Picha na Wizara ya Madini

Muktasari:

  • Kwa upande wake, ofisa madini mkazi mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Nkyando alisema soko hilo litasaidia kuboresha huduma za biashara ya madini kwa wafanyabiashara kupata sehemu sahihi za upatikaji wa madini ya aina mbalimbali

Hai. Serikali wilayani Hai mkoa wa Kilimanjaro imedhamiria kuanzisha soko la madini katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ili kuwa sehemu ya uhakika ya kuuzia madini ya aina mbalimbali kwa bei elezekezi

Akikagua eneo litakapojengwa soko hilo juzi, mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya alisema uanzishwaji wa masoko ya madini ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Januari 22 mwaka huu kwenye mkutano wake na wachimbaji wa madini nchini jijini Dar Es Salaam

Alisema soko hilo la kisasa litakuwa na aina zote za madini yanayopatikana Tanzania na litawasaidia wachimbaji wadogo kutambua bei elekezi ya Serikali ya ununuzi madini hayo hivyo kunufaka nayo na taifa kwa jumla.

“Soko hili kwa sasa tutalianzisha ndani ya uwanja huu wa ndege wa KIA na tunatarajia ndani ya siku saba litakuwa limekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wachimbaji.”

“Eneo linapoanzishwa soko hili la wilaya ni muhimu kutokana na kutumiwa na watalii wengi ambao hutumia usafiri wa ndege hivyo pia watapata fursa ya kutambua madini ya aina mbalimbali yanayopatikana hapa nchini,” alisema.

Ole Sabaya alisema kuwa soko hilo la madini litarahisisha huduma za uuzaji na ununuzi wa madini, ambapo huduma zote zitatolewa ndani ya jengo moja hivyo kuokoa muda wa wauzaji na wanunuzi.

Kwa upande wake, ofisa madini mkazi mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Nkyando alisema soko hilo litasaidia kuboresha huduma za biashara ya madini kwa wafanyabiashara kupata sehemu sahihi za upatikaji wa madini ya aina mbalimbali

Naye meneja biashara na masoko wa kampuni inayoendesha uwanja huo (Kadco), Christina Mwakatobe alisema uamuzi wa Serikali wilaya ya Hai kuweka soko hilo uwanjani hapo ni sahihi na kwamba utawasaidia kuongeza kipata cha wananchi na hasa wachimbaji wadogo wa mji mdogo wa Mirerani ambao madini ya Tanzanite yanapatikana eneo hilo pekee duniani.

“Soko hili la madini litasaidia sana kuongeza kipato cha wanajamii pamoja na nchi kwa ujumla, uwanja huu hutumiwa na wageni wa aina mbalimbali wa ndani na kutoka nje ya nchi hivyo watapata fursa ya kuona na kununua madini yanayotokana na nchi yetu,” alisema Mwakatobe.

Katika siku za hivi karibuni, masoko ya madini yamekuwa yakifunguliwa katika maeneo mbalimbali nchini zinakopatikana rasilimali hizo ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kutaka kuanzishwa masoko hayo ili sekta ya madini inayotegemewa kuchangia pato la taifa iweze kuleta tija kiuchumi na kuwanufaisha Watanzania wote.