Malawi kufanya uchaguzi wa marudio Julai 2

Wednesday March 25 2020

 

Lilongwe, Malawi. Uchaguzi wa marudio kwa ajili ya nafasi ya urais nchini Malawi unatarajia kufanyika Julai 2.

Uchaguzi huo unarudiwa baada ya Mahakama ya Kikatiba nchini humo kutengua matokeo yaliyompa ushindi Rais, Peter Mutharika.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Jane Ansah kupitia tangazo lake kwa vyombo vya habari alisema “kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Katiba ya Februari 3 yaliyofuta matokeo ya uchaguzi wa urais na kuagiza kufanyika uchaguzi mpya kwa sababu ya dosari, natangaza kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika Julai 2.”

Mei 21, 2019 Mahakama hiyo ya Malawi ilitangaza kutengua matokeo ya uchaguzi mkuu uliomrejesha madarakani Rais Peter Mutharika.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo ilisema matokeo ya uchaguzi huo kwa kiasi kikubwa yaligubikwa na udanganyifu na kuagiza kurudiwa katika kipindi cha siku 150.

Hata hivyo, Rais Mutharika alipinga hukumu hiyo na kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba uliomvua madaraka.

Advertisement

Katika hoja zake, Rais Mutharika alidai kuwa hukumu hiyo ilikuwa na upotoshaji wa haki na shambulio dhidi ya misingi ya demokrasia nchini Malawi.

Aidha, Rais huyo alisema kuwa kurudia uchaguzi ni gharama kubwa hivyo hakukuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Rufaa hiyo iligonga mwamba baada ya Mahakama kutupilia mbali hoja za Rais Mutharika.

Kwa mujibu wa Mahakama hiyo ya Rufaa nchini humo, demokrasia ni gharama hivyo wananchi wana haki ya kurudia uchaguzi.

Katika kile kinachoonyesha wazi kutokubaliana na uamuzi huo kiongozi huyo amewasilisha rufaa yake katika mahakama ya juu zaidi ambayo imepangwa kusikilizwa Aprili 15 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Awali vyama vya upinzani nchini huno vilifungua kesi Mahakama ya Kikatiba kupinga ushindi huo baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi Mei mwaka jana.

Majaji watano wa mahakama hiyo walisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro kadhaa ikiwamo matumizi ya wino bandia hivyo ushindi wa Mutharika haukuwa halali.

Akizungumzia hukumu hiyo, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo, Lazarus Chakwera alisema hukumu hiyo ni ukomboni kwa Afrika.

Advertisement