Ujerumani yaiomba radhi mauji Vita ya Pili ya dunia

Muktasari:

Taifa hilo limeiomba radhi Poland ikiwa ni miaka 80 tangu kutokea kwa Vita ya Pili ya dunia iliyosababisha uvamizi na mauaji ya zaidi ya watu milioni 50.

Warsaw, Poland. Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier ameomba msamaha kutokana na uvamizi na mauaji yaliyofanywa na Wanazi wa Ujerumani nchini Poland wakati wa Vita ya Pili ya dunia.

Steinmereier aliyasema hayo jana Jumapili Agosti Mosi wakati wa sherehe za kumbukumbu ya miaka 80 ya vita vya pili vya dunia ambazo zilifanyika mjini hapa.

“Nchi yangu ilifungua mnyororo wa vita mbaya ambayo ingegharimu maisha ya watu milioni 50, wakiwamo raia wa Poland,” alisema Rais Steinmeier aliponukuliwa na Shirika la habari la DW.

Rais Steinmeier alisema vita hiyo ilikuwa ni makosa ya Ujerumani hivyo aliwaomba msamaha wananchi wa Poland kwa mauaji yaliyotokea wakati wa mapigano hayo.

Rais wa Poland Andrzej Duda, Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Ufaransa, Edouard Phillipe pamoja na wawakilishi wa nchi nyingine 30 walihudhuria hafla hiyo.

Katika hotuba yake, Rais Duda alizungumzia uvamizi wa Ujerumani lakini pia mauaji ya kimbari ya kisovieti dhidi ya maofisa wa Poland mjini Katyn mwaka 1940 pamoja na mauaji katika makambi ya Wanazi.