Mamia ya wananchi Iran waandamana kuipinga serikali yao

Muktasari:

  • Wananchi wa Iran jana waliandamana kupinga kitendo cha serikali yao kuitungua ndege ya abiria na kuua watu 176 waliokuwemo katika ndege hiyo. wamewataka viongozi wa serikali kujiuzulu nyadhifa zao na waliohusika na utunguaji huo kuchukuliwa hatua mara moja.

Tehran. Muda mfupi baada ya Serikali ya Iran kukiri kuitungua ndege kwa bahati mbaya, kundi la waandamanaji nchini humo limejitokeza kutaka kiongozi wa juu, Ayatollah Khamenei pamoja na viongozi wengine waandamizi kujiuzulu nyadhifa zao.

Ndege aina ya Boeing 737-800, mali ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Ukraine (UIA) ilitunguliwa Jumatano iliyopita wakati Iran ikishambulia kambi za kijeshi za Marekani zilizopo Iraq kwa lengo la kulipa kisasi baada ya kuuawa kwa kamanda wake, Qasem Soleimani.

Nchi za Marekani na Canada zilieleza kwamba ndege hiyo iliyokuwa na watu 176 ilitunguliwa na makombora ya Iran wakati wakilenga kuzishambulia kambi za jeshi la Marekani. Baadaye, serikali ya Iran ilikiri kuitungua ndege hiyo kwa bhati mbaya.

Baada ya serikali ya Iran kukiri kutenda kosa hilo, wananchi wake walianza kuandamana sehemu mbalimbali wakiikosoa serikali yao na kuwataka viongozi wake wa juu kujiuzulu nyadhifa zao mara moja.

“Amiri Jeshi Mkuu (Khamenei) jiuzulu, jiuzulu,” video iliyopostiwa kwenye mtandao wa Twitter ilionyesha mamia ya waandamanaji wakiimba mbele ya Chuo Kikuu cha Amir Kabir kilichopo mjini Tehran.

Waandamanaji hao waliwaita viongozi wa Iran “waongo” na kushinikiza wajiuzulu huku wale waliohusika kuitungua ndege hiyo waadhibiwe kwa kosa hilo na kuficha taarifa za kitendo hicho kilichogharimu maisha ya watu kutoka mataifa mbalimbali.

Shirika la habari la Fars liliripoti kwamba jeshi la polisi liliwatawanya wanafunzi ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kuwakashifu viongozi wa taifa hilo kutokana na kitendo cha kuangushwa kwa ndege hiyo.

Uingereza ilithibitisha kukamatwa kwa balozi wake nchini Iran, Rob Macaire kwa madai kwamba alikuwa anachochea maandamano ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Amir Kabir. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab alisema kukamatwa kwa balozi huyo ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Rais wa Marekani ameandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema Marekani inafuatilia kwa karibu maandamano ya Iran na kwamba wamevutiwa na ujasiri wa watu wa Iran ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida.

“Serikali ya Iran lazima iruhusu vikundi vya haki za binadamu kufuatilia na kuripoti ukweli halisi juu ya maandamano yanayoendelea ya watu wa Iran. Hakuwezi kuwa na mauaji mengine ya waandamanaji wa amani, wala kuzimwa kwa mtandao. Ulimwengu unaangalia,” ameandika Trump katika ukurasa wake wa Twitter.