Waliokufa katika ndege Congo wafikia 24

Muktasari:

Ni baada ya ndege iliyokuwa imebeba abiria 17 kuanguka wakati ikiruka na kuua abiria wote waliokuwamo pamoja na wengine kadhaa waliokuwa eneo la tukio.

Goma, DRC. Idadi ya watu waliofariki dunia baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kuangukia katika mji wa Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefikia 24.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka watu 18 wakiwamo wafanyakazi wawili wa ndege hiyo walioripotiwa kufa muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.  

Ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 17 imeanguka jana Jumatatu Novemba 24 wakati ikiruka na kuua abiria wote waliokuwamo.

Makamu wa rais wa Bunge la Kivu Kaskazini, Jean Paul Lumbulumbuis alisema miili 24 imepatikana kwenye vifusi ikiwamo ya watu kadhaa waliokuwa eneo la tukio.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa taasisi ya uokoaji ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema miili ya watu 26 imepatikana katika eneo la tukio.

Awali Gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Nzanzu Carly alisema kuna watu wamefariki katika ajali hiyo lakini hakutoa idadi kamili.

Ndege hiyo ilianguka juu ya nyumba katika eneo jirani la Mapendo baada ya kushindwa kupaa katika uwanja wa ndege wa mji huo, alisema akinukuliwa na CCM.

Wakazi wa eneo hilo ni miongoni mwa waathiriwa wa ajali hiyo, kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilo.

Ndege hiyo aina ya Doenier 228 ilikuwa ikimilikiwa na kampuni binafsi ya Busy Bee. Ilitarajiwa kuelekea Beni, umbali wa kilomita 350 kutoka kaskazini mwa Goma wakati ilipoanguka dakika moja baada ya kupaa.

Ajali za ndege hutokea mara kwa mara nchini DRC kutokana na viwango vya chini vya usalama na kutorekebishwa kwa ndege hizo.

Ndege zote za kibiashara za Taifa hilo zimepigwa marufuku kufanya biashara katika Muungano wa Ulaya.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulisema kuwa umetuma kikosi cha uokozi kwenda eneo la tukio pamoja na magari mawili ya kuzima moto ili kusaidia mamlaka nchini humo.

Ajali za ndege hutokea mara kwa mara nchini DRC kutokana na matengezo hafifu ya ndege na kiwango cha chini cha usalama kwenye usafiri wa anga.

Mwezi Oktoba, ndege ya mizigo iliyokuwa safarini kutoka Goma kuelekea mji mkuu Kinshasa ilianguka nusu saa baa da ya kuruka angani katika mkoa wa kati nchini Congo wa Sankuru, na kuwauwa abiria wote wanane na wahudumu.

Kwenye orodha yake ya mashirika ya ndege yaliyopigwa marufuku kuhudumu barani Ulaya, Umoja wa Ulaya umeyaorodhesha mashirika 21 ya Congo, likiwamo la Busy Bee.