Wapinzani Hong Kong washinda kwa kishindo serikali za mitaa

Muktasari:

Wapigania demokrasia visiwani Hong Kong wamenyakua wilaya 17 kati ya 18.

Hong Kong, China. Kambi ya wapigania demokrasia visiwani Hong Kong imeibuka kidedea katika uchaguzi wa viongozi wa halmashauri za mitaa.

Kiongozi wa wapigania demokrasia hao, Carrie Lam katika taarifa yake alisema kwamba matokeo hayo yanaashiria wananchi kutoridhishwa na uongozi wa mji huo.

Kiongozi huyo alisema Serikali anaamini Serikali itasililiza kwa unyenyekevu na kutafakari sana juu ya uchaguzi huo na kuchukua hatua.

Uchaguzi wa halmashauri za mitaa umekamilika visiwani Hong Kong Jumatatu iliyopita ambako vyama vinavyounga mkono demokrasia vimeshinda katika halmashauri wilaya 17 kati ya 18 za jiji hilo.

Akizungumza kuhusu uchaguzi huo, Kevin Lam ambaye ni mshindi wa halmashauri ya Wilaya ya South Horizons West alisema matokeo hayo yanaashiria ujumbe wa wananchi kwa Serikali kuu ya China pamoja na viongozi wa Hong Kong.

"Kwamba wapiga kura hawafurahishwi na jinsi Serikali inavyoshughulikia waandamanaji hususan katika miezi mitano iliyopita na ukatili wa polisi ulivyoathiri wananchi. Wananchi wa Hong Kong wanapaswa kutumia matokeo haya kudai demokrasia zaidi siku za usoni,” alisema Lam.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje, Wang Yi alisema Hong Kong bado ni sehemu China bila ya kujali kinachotokea katika eneo hilo lenye mamlaka yake ya ndani.

Wang alisema hayo wakati akizungumza na waandishi habari mjini Tokyo, Japan na kuongeza kuwa jaribio lolote la kuharibu utulivu na maendeleo ya Hong Kong haliwezi kufanikiwa.

Awali Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe ambaye alikutana na Wang alisisitiza umuhimu wa kuwapo Hong Kong iliyo huru na yenye uwazi chini ya mfumo wa nchi moja lakini ikiwa na Serikali mbili.

Wakati huo huo, Serikali ya Taiwan ilisema matokeo hayo yanaonyesha azma ya wananchi ya kutafuta demokrasia na uhuru huku viongozi kadhaa wa Marekani wakiwamo wanasiasa mashuhuri wa vyama vya Democratic na Republican, pamoja na maseneta Marco Rubio na Elizabeth Warren wamesifu matokeo hayo.

Matokeo hayo yanaweza kuilazimisha Serikali kuu ya China kutafakari tena jinsi ya kushughulikia maandamano ambayo kwa sasa yanatimiza miezi sita.

Waandamanaji hao pamoja na mambo mengine, wanapinga kitendo cha Serikali kuu kuingiliaji uhuru wa visiwa hivyo na kushinikiza kuachwa wajisimamie wenyewe.