Waziri Mkuu mpya ateuliwa Urusi

Thursday January 16 2020

 

Moscow, Urusi. Siku moja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev kujiuzulu chama tawala nchini humo cha United Party kimempitisha kwa kauli moja Mikhail Mishustin kuziba nafasi hiyo.

Hata hivyo, uteuzi wa waziri mkuu huyo utakamilika baada ya bunge la nchi hiyo kumpigia kura baadaye leo.

Waziri Mkuu, Medvedev alitangaza kujiuzulu jana pamoja na Serikali yake baada ya Rais Vladimir Putin kupendekeza mageuzi ya Katiba yenye lengo la kumwezesha kuendelea kuwa na ushawishi wa kimamlaka hata baada ya kuondoka kwenye wadhifa wake.

Medvedev ametangaza kujiuzulu akisema kuwa yeye pamoja na serikali anayoiongoza inaachia ngazi ili kumpa nafasi Rais Vladmir Putin kufanya mabadiliko ya Katiba

Medvedev aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Putin Jumatano jioni kisha kutoa tamko hilo kupitia Televisheni ya Taifa ya Urusi akiwa ameketi sambamba na Rais Putin ambaye ni mshirika wake wa karibu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Urusi, Putin amemshukuru waziri mkuu huyo aliyejiuzulu kwa utumishi wake huku akibainisha kuwa baraza lake la mawaziri lilishindwa kutimiza majukumu yake.

Advertisement

Advertisement