Waziri Mkuu wa Uingereza aendelea kuwa ICU kwa siku ya pili

London. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ametumia siku ya pili akiwa chumba cha uangalizi maalum wa matibabu (ICU) akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Covid-19.

Boris ambaye alibainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona Machi 27 alipelekwa katika hospitali ya St Thomas Aprili 5 kwa vipimo zaidi baada ya hali yake kubadilika na Aprili 6 akapelekwa ICU.

Kwa mujibu wa Shirikia la Utangazaji Uingereza (BBC) limeripoti Waziri wa Afya, Edward Argar amesema hali ya Boris inaendelea vizuri.

“Ametulia, anaimarika na ana imani kubwa,” amesema Argar

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje, Dominic Raab ambaye pia ana kaimu nafasi ya Boris amesema amekuwa akijiamini huku akimuita ni mpambanaji.

Raab amesema Boris amepatiwa matibabu ya hewa ya oxygen na akawa anapumua bila msaada wowote kama vile mashine ya upumuaji.

Raab amehakikisha kuwa Waziri Mkuu amekuwa akipata uangalizi mzuri wa kitabibu hospitalini hapo.

Raab ameeleza Boris sio kiongozi tu kwake bali ni rafiki amemuombea rafiki yake huyo na familia yake kwa ujumla.

Malkia wa Uingereza Elizabeth II na viongozi wa juu walimtumia salamu za pole Boris na mchumba wake ambaye ni mjamzito na kumtakia apone haraka