Aliyetumwa na Lissu kuchukua vifaa alituhumu Bunge

Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Dodoma. Amina Abrahaman, ambaye aliagizwa na mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kufuatilia vifaa vilivyo kwenye nyumba yake jijini Dodoma, amesema ofisi ya Bunge haimpi ushirikiano kufanikisha kazi hiyo.

Tangu ashambuliwe kwa risasi akiwa jijini Dodoma miaka mitatu iliyopita na kupelekwa Kenya na baadaye Ubelgiji kwa matibabu, Lissu hajarudi nchini.

Alipigwa risasi takriban 30 akiwa ndani ya gari nje ya makazi yake jijini Dodoma na mwaka jana Spika Job Ndugai alitangaza kumvua ubunge kwa maelezo kuwa haonekani bungeni na hajajaza fomu za mali na madeni, lakini mwanasheria huyo amesema anasumbuliwa kuchukua vifaa vyake vilivyoko katika nyumba hiyo.

Wiki iliyopita aliiambia Mwananchi kuwa mtu aliyemtuma na kumtaja kwa jina la Amina bado hajapewa vifaa hivyo, lakini katibu wa Bunge aliiambia Mwananchi kuwa aliyetumwa hapatikani.

Lakini jana Amina aliiambia Mwananchi kuwa mara ya kwanza alikwenda ofisi za Bunge kwa lengo la kuwaeleza wamfungulie nyumba ili kutoa vitu vya bosi wake na akaambiwa awasiliane na Lissu ili aliandikie barua Bunge.

Alisema baada ya Lissu kuandika barua hiyo, alipigiwa simu na mmoja wa watumishi wa Bunge aliyemtaka akatoe vitu hivyo.

“Niliomba msaada wa vijana wa kanda (ofisi ya Chadema, Kanda ya Kati) ili wakanisaidie, lakini nilipofika wale watu (watumishi wa Bunge) walikuwa wameondoka kwa maelezo kuwa wana vikao, “ alisema.

“Niliwaomba funguo wakasema hawawezi kunipa hadi wawepo.

“Imekuwa vigumu kwenda kuvitoa vitu kwani niliwaambia Jumatatu hadi Ijumaa ni ngumu lakini Jumamosi au Jumapili inawezekana (anamtaja mtumishi wa Bunge) yeye anasema Jumamosi wana vikao na Jumapili anapumzika, sasa hapo ndipo kuna shida, ninasubiri Bunge limalizike nifuatilie tena.”

Jana, Lissu alisema vitasa vya milango katika nyumba hiyo iliyoko Area D jijini Dodoma vimebadilishwa jambo linalomtia wasiwasi kuhusu kupata mali zake ambazo ni pamoja na mabegi yenye nguo zake, viatu, vitabu, jiko la gesi na friji.

Nyumba hiyo alipangishiwa na Bunge alipokuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani na baada ya Juni 28 mwaka jana kuvulia ubunge, ofisi ya Bunge ilibadilisha vitasa.

hakuna mtu anaishi katika nyumba hiyo iliyopo jirani na Shule ya Msingi ya Mlimwa. Lissu alisema Amina amekuwa akizungushwa na uongozi wa Bunge kila alipotakiwa na Lissu kwenda kuonana nao ili kupewa mwongozo wa kutoa vitu kwenye nyumba hiyo.

Lissu alipoteza ubunge baada ya Spika Job Ndugai kusema hajatoa taarifa ya wapi alipo na kutokujaza fomu za mali na madeni ya viongozi wa umma.

Lissu amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7 mwaka 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana. Siku hiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi akitokea Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Januari 6 mwaka 2018, Lissu alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi na mpaka sasa amekwisha kumaliza matibabu anasubiri kuhakikishiwa usalama wake ili arejee nchini.

Desemba 30 mwaka jana, Lissu aliandika barua kwenda kwa Katibu wa Bunge akimuomba amruhusu Amina kuondoa vitu kwenye nyumba hiyo.

“Wawafungulie ndugu zangu nyumba hiyo ili kuwawezesha kutoa vitu vyote ambavyo ni mali yangu binafsi. Namuelekeza Amina Abrahamani ambaye alikuwa mtumishi wangu kwenye nyumba hiyo kutoa vitu hivyo na kuvikabidhi kwa ndugu zangu. Nashukuru kwa ushirikiano wako kwenye jambo hili,” alieleza Lissu kwenye barua hiyo.

Lissu alilieleza Mwananchi kuwa vitu vilivyopo katika nyumba hiyo ni, “ni vitu vingi sana. Baadhi ni Mabegi ya mavazi, viatu, vitabu, jiko la gesi, friji vyote vinahitaji maboksi zaidi ya kumi.”

Akizungumzia suala hilo, katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai alisema wameipata barua ya Lissu ya kuomba kutoa vitu vyake lakini mtu aliyeelekeza afunguliwe mlango bado hajapatikana.

“Tumeshaipata barua lakini tumemtafuta mtu aliyeeleza afunguliwe mlango ili achukue vitu vyake hatujafanikiwa kumpata,” alisema Kagaigai.

Alisema kuna wakati alisema angefika lakini walimsubiri hakutokea na kwamba wamejaribu hata kutumia viongozi wa Chadema, lakini hawakufanikiwa kumpata.

Lakini Lissu alisema:“Katibu amefuatwa na mwenyekiti (wa Chadema, Freeman) Mbowe (Freeman), (mbunge wa Tarime Mjini) Esther Matiko pamoja na dada Amina, lakini hawajafanikiwa.”