Chadema wajifungia siku mbili kutafakari uchaguzi mkuu, Tume huru ya uchaguzi

Sunday February 16 2020

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wajumbe Kamati Kuu ya Chadema wamekutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam wakitafakari Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, huku suala la kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi likibaki kuwa kitendawili.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene juzi ilisema kikao hicho cha siku mbili kinalenga kujadili hali ya kisiasa nchini na maandalizi ya uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais.

Mwananchi ilijaribu kuzungumza jana na wajumbe hao waliiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe katika hoteli ya Bahari Beach Ledger Plaza jijini Dar es Salaam unapofanyikia mkutano huo, lakini hata hivyo hawakutaka kueleza kwa undani juu ya ajenda za kikao chao.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alipoulizwa baadaye aliahidi taarifa rasmi itatolewa, lakini yanayojadiliwa ni hali ya siasa nchini na uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Februari 3, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa chama hicho kimemwandikia barua Rais John Magufuli kikimwomba aunde kamati ya maridhiano ya kisiasa, pia kilitaka kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi na kurudiwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka jana.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Januari 29, mwaka huu, Chadema wamehoji kutumiwa kwa wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi, huku pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiwa na uongozi ulioteuliwa na Rais, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.

Advertisement

Suala la kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi pia lilitajwa katika vipaumbele vya Katibu mkuu, John Mnyika baada ye kuteuliwa, na vilevile limetajwa hivi karibuni katika tamko lililotolewa na Ubalozi wa Marekani, Januari 31, mwaka huu.

Katika tamko hilo, Marekani ilimpongeza Rais Magufuli kwa kuwahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki, lakini pia ubalozi huo ukamtaka Rais kuhakikisha Tume huru ya uchaguzi inapatikana.

Januari 21, mwaka huu, Rais John Magufuli aliwahakikishia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki alipokuwa akizungumza nao katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akisisitiza madai hayo, Februari 6, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa upinzani bungeni alimuuliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu kupatikana kwa Tume huru ya uchaguzi na hatua ya vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

“Ni lini Serikali itaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi ili kujiandaa na uchaguzi mkuu na Serikali ina mpango gani wa kuwezesha Taifa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ili uchaguzi uwe wa haki na halali?”

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Majaliwa aliitetea Tume ya Uchaguzi akisema imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na haiwezi kuingiliwa na mamlaka yoyote.

“Tume hii imeundwa kwa mujibu wa Katiba, kipengele cha 74(7,11, 12) kinachoeleza kuwa hicho ni chombo huru. Imeelezwa kwenye Katiba kinaundwaje chombo hiki na kuwa hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote, iwe Rais, iwe chama chochote cha kisiasa au mamlaka yoyote nyingine haipaswi kuingilia. Kama ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba ndiyo tume huru,” alisema Majaliwa.

Kuhusu madai ya vyama vya siasa kuzuiwa kufanya siasa, Majaliwa alikanusha madai hayo akisema kilichofanywa ni kuwekwa kwa utaratibu.

Chadema pamoja na baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika hali ya siasa nchini ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kwa zaidi ya miaka minne sasa.

Miongoni mwa shughuli za siasa zinazotajwa kuzuiwa ni pamoja na maandamano yaliyotarajiwa kufanywa na Chadema, Septemba 30, 2016 yaliyopewa jina Ukuta.

Mbali na kuzuiwa kwa maandamano hayo, viongozi wa vyama vya upinzani wamejikuta matatani kwa kukamatwa na kufunguliwa kesi na huku wengine kufungwa jela.

Mpaka sasa viongozi tisa wa Chadema wakiwemo wabunge wanaendelea na kesi ya jinai yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Chanzo cha kesi hiyo ni maandamano yaliyofanya Februari 15, 2018 ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, ambapo walikuwa wakipinga hatua ya msimamizi wa uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuwanyima fomu mawakala.

Kutokana na hali hiyo, kwa vyovyote vile kikao hicho hakiwezi kumalizika bila kujadili suala la Tume huru ya uchaguzi.

Advertisement