China, Tanzania waanzisha ushirikiano wa asasi za kiraia

Balozi wa China Tanzania, Wang Ke;

Muktasari:

Tanzania na China zimeanzisha ushirikiano wa asasi za kiraia kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika mkakati wa kukuza urafiki wa mataifa hayo ulioanza miaka 60 iliyopita.

Dar es Salaam. Tanzania na China zimeanzisha ushirikiano wa asasi za kiraia kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika mkakati wa kukuza urafiki wa mataifa hayo ulioanza miaka 60 iliyopita.

Sherehe za uzinduzi wa mpango wa ujenzi wa jumuiya umefanyika leo Alhamisi Desemba 19, 2019 jijini Dar es Salaam ambapo asasi za kiraia za Tanzania na China zimesaini hati za makubaliano.

Hafla ambayo imeshuhudiwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai; Balozi wa China nchini, Wang Ke;  Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki na wawakilishi wa asasi mbalimbali za kiraia.

Akizungumzia ushirikiano huo, Spika Ndugai amesema ushirikiano wa asasi hizo za kiraia ni muhimu, unatakiwa kuendelezwa kwa manufaa ya wananchi hasa wa Tanzania.

Amezitaka asasi za kiraia za China mbali ya kutoa msaada wa fedha na vitu, zitoe msaada wa kiufundi na teknolojia. Amesema asasi za Tanzania  zina mengi ya kufundisha kama urithi wa utamaduni.

“Huko nyuma tulizoea ushirikiano wa Serikali na serikali, sekta ya biashara kwa biashara lakini sasa tunashuhudia ushirikiano wa asasi za kiraia. Hili ni jambo muhimu kwa sababu wanafanya kazi kwa karibu na wananchi,” amesema Ndugai.

Balozi Ke amesema ushirikiano huo ni mwendelezo wa azma ya Rais wa China, Xi Jinping kuimarisha uhusiano wa China na bara la Afrika katika masuala ya maendeleo.

“Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mshikamano wa watu wetu na ubadilishanaji wa tamaduni kati ya nchi zetu mbili. Watanzania wengi wana ari ya wanakwenda kusoma China, vyuo vingi vya China vinafundisha lugha ya Kiswahili,” amesema Ke.

Mwenyekiti wa chama cha kuendeleza urafiki wa China na Tanzania (TCFPA), Dk Salim Ahmed Salim akiwakilishwa na katibu mkuu wa chama hicho, Joseph Kahama amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha urafiki kati ya mataifa hayo.