Lema afikishwa mahakamani, asomewa mashtaka 15

Muktasari:

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Singida na kusomewa mashtaka 15 yanayomkabili.

Singida. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Singida na kusomewa mashtaka 15 yanayomkabili.

Kati ya mashtaka hayo moja ni la kusababisha taharuki kwa jamii na 14 ya kupotosha jamii.

Amesomewa mashtaka hayo leo Jumatano Machi 25, 2020 na mawakili wa Serikali, Monica Mbogo, Rose Cholongola, Michael Ng’hoboko na Caren Malando mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Consolata Singano.

Imeelezwa kuwa Lema alitenda kosa hilo  Februari 29, 2020 mjini Manyoni mkoani Singida katika mazishi ya kiongozi wa Chadema.

Anadaiwa siku hiyo na katika mitandao ya kijamii alisambaza taarifa za uongo kwa nia ya kupotosha jamii kuwa watu 14 wameuawa kwa kupigwa mkoani Singida.

Lema alikana mashtaka yote yanayomkabili na shauri hilo kuahirishwa hadi Aprili 15, 2020 huku mbunge huyo akiachiwa kwa dhamana.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi