TUONGEE KIUME: Michepuko mjiongeze kidogo

Sunday September 8 2019

 

Tazama mfano huu.

Umerudi kazini, umekaa na mama watoto, kashika simu yake kageukia kule, wewe umeshika yako umegeukia huku unaperuzi mtandaoni. Mara unakumbana na kavideo fulani hivi kanakuvutia, unakatazama kanakuchekesha, unacheka sana, sana kama mwenda wazimu hadi machozi yanakutoka. Unasema hapana, hii kitu lazima na mke wangu naye aone tucheke pamoja.

‘Njoo uone’ unamuita. Anakugeukia, anasogea karibu yako, unamsogezea simu unamuonyesha ulichokuwa unaangalia. Video inaanza, sekunde ya kwanza, ya pili, ya tatu, mara kinaingia kimeseji wakati video inaendelea na kama unavyojua ‘smartphone’, meseji ikiingia, hata kama unafanya vitu vingine kwenye simu, yenyewe inajitokeza pale kwa juu ikionesha jina la aliyeituma na alichokiandika.

Basi, kwa sababu Mungu aliwapendelea wanawake vipaji vya kufanya mambo mawili mawili kwa wakati mmoja; mkeo kwa wakati huo huo anaotazama video unayomuonyesha, anasoma jina la mtumaji na meseji... baby kesho usinidanganye kama leo meseji kutoka kwa Jack Sinza.

Kuanzia hapo hakuna tena video ya kuchekesha, sebule inachafuka, mambo yanaharibika, nyumba inawaka moto, mzee unawekwa kizimbani ujitetee utetezi ambao hata ukinena kwa lugha haitatokea ueleweke.

Kusuluhisha

Advertisement

Kesi kama hizi zinatukuta, na ni ngumu sana kupata suluhisho zikishatokea, kwa hiyo unachohitaji ni kinga tu, ni kuhakikisha hazitokei. Na kuna njia mbili za kujikinga nazo.

Ya kwanza ni kujiongeza wewe na mchepuko wako, mkawekeana sheria na mipaka ya mawasiliano, mfano kwamba ikifika saa 2 usiku mwisho wa kupigiana simu na kutumiana meseji.

Na kama kukiwa na shida ambayo anaona ni lazima muwasiliane, basi mnaweza kuwa hata na meseji ya kuzuga. Kwa mfano, ikishafika saa 2 usiku, akitaka kukupigia au kukutumia meseji aanze kwa kuandika ‘Naweza kupata kazi hapo ofisini kwenu? ukijibu Sawa. Nitakujulisha zikitokea. Ajue kuwa ulipo, hakuna usalama kwa wakati huo.

Yaani kwa kifupi, hapa cha kulinda ni simu tu kwa sababu matatizo yote yanaanzia hapo siku hizi. Ndiyo maana kuna wanaoenda kuoga na simu au wanazificha, hazionekani hadi watoke bafuni. Wengine simu zina nywila ngumu kama zimeficha mafaili ya siri ya ufisadi wa EPA. Wengine wana ‘laini’ maalum ya michepuko, akiingia nyumbani anaitoa kwenye simu... Yaani ni shida tu.

Sasa kama hutaki purukushani zote hizo tumia njia ya pili ambayo ni kutokuwa na mchepuko kabisa ukiweza hii, magonjwa ya moyo, na presha presha za ajabu zitachelewa sana kukupata kwa sababu utakuwa na amani muda wote, unajiamini hakuna cha ajabu atakachokiona.

Advertisement