Robert Mugabe alikufa na kinyongo

Harare, Zimbabwe. Wakati ratiba ya mazishi ya Rais wa zamani wa Zimbabwe ikitolewa, wanafamilia wa kiongozi huyo wamedai kuwa baba yao amekufa na uchungu moyoni.

Mpwa wa kiongozi huyo, Leo Mugabe alisema Rais Mugabe alikuwa akisononeka kuhusu Taifa hilo lilivyomgeuka.

Mugabe, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 Ijumaa iliyopita, aliongoza Zimbabwe kwa miaka 37 kabla ya kung’olewa na jeshi la nchi hiyo mwaka 2017.

“Fikiria watu uliowaamini. Watu ambao walikuwa wakikulinda, wakikufuata lakini wanakugeukia.

“Alikuwa na uchungu sana na ilionyesha hata katika urithi wake. Haikuwa jambo rahisi kwake kuchukua,” alisisitiza mpwa huyo alipozungumza na Shirika la habari la (BBC) kutoka.

Katika hatua nyingine, mwili wa Rais huyo wa zamani unatarajiwa kuzikwa Jumamosi nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na familia ya kiongozi huyo, inasema kuwa tayari maafisa wa Serikali wakiambatana na wanafamilia wamekwenda nchini Singapore kwa ajili ya kuchukua mwili.

Rais Mugabe alifariki dunia wiki iliyopita nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuuga kwa muda mrefu.

Taarifa ya familia hiyo iliyotolewa na mpwa wa kiongozi huyo, ilisema ujumbe huo umeondoka mjini Harare jana asubuhi na ndege maalumu na kutarajiwa kurudi na mwili wa Mugabe Jumatano mchana.

“Utakapowasili, mwili utapelekwa kijijini kwake Zvimba kilichopo kilomita 90 Magharibi mwa mji mkuu wa Harare kwa ajili ya mkesha.

“Alhamisi na Ijumaa utawekwa katika Uwanja wa Rufaro kitongoji cha Mbare ili wananchi wamuage kisha kurejeshwa mjini Harare kabla ya maziko rasmi yatafanywa Jumamosi katika Uwanja wa wa Taifa wa Zimbabwe wenye viti 60,000.