Breaking News

Wadau wajikite katika elimu ya mpigakura

Sunday October 18 2020

 

Tukiwa tumebakiza siku tisa kufikia Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani, vyama vya siasa na wagombea wanaendelea kujinadi na kufanya kila wawezalo kushawishi wapigakura.

Kwa takriban siku 50 zilizopita tangu kampeni zilipoanza tumeshuhudia jinsi viongozi, wafuasi na wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa walivyokuwa wanapita na kujenga hoja kutafuta uungwaji mkono.

Baadhi yao walifanikiwa kuvifikia vyombo vya habari, mabango, vipeperushi na wengine wakatumia mitandao ya kijamii, achilia mbali wale waliotumia mikutano ya hadhara, vijiwe na mikusanyiko ya kila aina ilimradi waweze kuwafikia wapigakura na kuwaomba kura.

Pamoja na kwamba wahusika hao bado wana jukumu la kufanya kampeni za lala salama, tunadhani pia wanao wajibu wa kutoa elimu sahihi ya mpigakura na elimu ya uraia ili wale watakaojitokeza kupiga kura waelewe nini cha kufanya.

Ni matarajio yetu kwamba kwa muda uliosalia wanasiasa na wadau wengine wa uchaguzi walioruhusiwa, watatumia kila wasaa wanaoupata kufafanua masuala mbalimbali yanayohusu upigaji kura, bila kusahau umuhimu wa watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Tunalisema hilo tukikumbuka matukio ya chaguzi za miaka ya nyuma ambapo watu waliojitokeza kupiga walikuwa chini ya matarajio.

Advertisement

Tena bahati mbaya kumekuwa na chaguzi ndogo ambazo hazikuwavutia wapiga kura wengi. Na waliojitokeza walikuwa chini ya asilimia 50 ya matarajio.

Vilevile, yapo masuala ambayo yasipofafanuliwa yanaweza kuwaathiri watu wengi na kujikuta wanaharibu kura au kusababisha usumbufu usio wa lazima.

Mathalani, wananchi wanatakiwa kujua utaratibu wa siku ya uchaguzi na wasimamizi wahakikishe unafuatwa kadri ulivyopangwa.

Tumeona karatasi za mfano za kupigia kura na wananchi wanatakiwa kuzifahamu mapema na alama zake ili wanapokwenda kupiga kura wasiwe wageni nazo.

Vilevile, kila mtu anayehusika na uchaguzi anatakiwa kujua wajibu wake na pia azifahamu haki zake, wakiwamo wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi ambao wanatakiwa wajue sheria wanazotakiwa kulinda na kutendewa haki kwa kila mhusika.

Hayo yote yanawezekana ikiwa kila mdau anayehusika na uchaguzi, atatumia muda uliosalia kwa umakini ili kuhakikisha elimu sahihi inamfikia kila mmoja.Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama mdau mkuu wa uchaguzi huo, nayo inatakiwa kutoka maudhui sahihi yanayopaswa kusambazwa ili ujumbe mahsusi uwafikie wananchi.

Pia ni kipindi ambacho NEC kama haijafanya hivyo, iwasisitize wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi, kusimamia sheria na kutenda haki katika maeneo yao ili wadumishe amani katika kipindi chote cha uchaguzi.

Mawakala wa wagombea nao waelimishwe mapema majukumu yao, nini wanatakiwa kuwa nacho, wanaapa wapi, muda gani, barua za utambulisho zinakuwaje na zinaandikwa na nani.

Hili ni eneo ambalo ni nyeti na kwa siku za karibuni limesababisha msuguano usiokuwa wa lazima.

Jambo jingine la msingi ambalo NEC inatakiwa kusisitiza kwa wasimamizi ni kuharakisha kutangaza matokeo pale kura zinapokamilika kuhesabiwa ili kuepusha mambo ambayo tuliwahi kushuhudia miaka ya nyuma.

Hata vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kupewa elimu ili maofisa wake wajue majukumu na mipaka yao katika uchaguzi.

Kwa upande wa Zanzibar ambako kura zinapigwa siku mbili, utaratibu ulio wazi unapaswa kujulikana ni nani wanaopiga kura ya mapema na usimamizi na ulinzi wa kura hizo utakuwaje ili kuepuka msuguano.


Advertisement