Watuhumiwa mauaji mwanaharakati walia kortini kunyimwa chakula

Friday January 17 2020

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mshtakiwa Nduimano Zebadayo na mwenzake ambao ni raia wa Burundi wameangua kilio mahakamani wakidai wananyanyaswa kutokana na uraia wao na kunyimwa chakula katika Gereza la Keko Dar es Salaam kwa  siku ya tano.

Zebadayo ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa kupambana na mauaji ya Tembo, Wayne Lotter ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 17, 2020 wakati  shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Awali, wakili wa Serikali, Ester Martin ameieleza Mahaka ya Hakimu Mkazi Kisuti Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Isaya kuwa shauri hilo limekuja kwaajili ya kutajwa na upelelezi uko hatua za mwisho na jalada liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)

Mshtakiwa huyo na mwenzake Habonimana Nyandwi wote ni raia wa Burundi wameondolewa kwenye orodha ya kupewa chakula katika gereza la Keko hivyo hadi leo ni siku ya tano hawajala.

Mshtakiwa huyo amedai hapa nchini hawana ndugu wa kuwaletea chakula na amedhoofu kutokana na kutopewa chakula katika gereza hilo.

Zebadayo amedai yeye na Nyandwi waliitwa na ofisa usalama wa gereza hilo na kuelezwa hawapo kwenye orodha ya kupewa chakula hivyo walitaka kuonana na mkuu wa gereza hilo lakini walizuiwa.

Advertisement

"Jana tulipata nafasi ya kuonana na mkuu wa gereza la Keko tulipomueleza alitujibu kwa nini tunyimwe chakula wakati ni majirani, hajui kinachoendelea huku chini  tumedhoofika kwa kukosa chakula na hatuna ndugu wa kutuletea chakula hivyo mimi na Nyandwi tumenyimwa chakula leo ni siku ya tano tunaiomba mahakama  itusaidie," amedai Zebadayo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu  Isaya alimtaka ofisa wa magereza kujibu hayo malalamiko ndipo ameieleza mahakama hana taarifa ya kunyimwa chakula kwa washtakiwa hao hivyo analifuatilia.

Isaya amesema anaahirisha shauri hilo kwa siku saba ili afuatilie  kama malalamiko yao yamefanyiwa kazi hivyo kesi hiyo imeahirisha hadi Januari 24, 2020.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji namba tisa ya mwaka 2017 ni Robert Mwaipyana, Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A. Inocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Wengine ni Meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B, Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B na Mohammed Maganga (61) mchimba makaburi, Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.

Katika kesi ya msingi washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, wanadaiwa kumuua Lotter.

Advertisement