Suma JKT wapewa kazi ujenzi hospitali Ubungo

Muktasari:

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) limepewa kazi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ubungo.

Dar es Salaam. Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) limepewa kazi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ubungo.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Oktoba 29, 2019 na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akibainisha kuwa ujenzi huo utafanyika kwa miezi mitatu.

Mkuu huyo wa Mkoa na watendaji wengine mkoani humo leo wametembelea eneo itakapojengwa hospitali hiyo ambako maandalizi mbalimbali yameanza kufanyika.

Makonda amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kukubali ombi lake la Sh1.5 bilioni za ujenzi wa hospitali hiyo.

"Wilaya hii ni mpya inahitaji viongozi shupavu wa kuwaletea maendeleo, hiyo ni kazi ya viongozi wanaochaguliwa na wananchi.”

“Kwa bahati mbaya Ubungo ilipata viongozi wanaojali matumbo yao tu. Hata leo hapa (eneo itakapojengwa hospitali) hawapo ila kesho watakuja na maneno matamu ili muwape kura," amesema Makonda.

Mkurugenzi mtendaji wa Suma JKT,  Kanali Rajabu Mabele amesema ujenzi huo utakamilika katika muda uliopangwa.