Mavunde atambua vipaji vya wanafunzi 21, awapa ufadhili wa masomo

Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Anthony Mavunde

Muktasari:

 Shindano la kuibua vipaji kwa wanafunzi wa shule za msingi jijini Dodoma nchini Tanzania limehitimishwa leo Jumatano Desemba 4, 2019 kwa shule ya msingi Chadulu kuibuka mshindi na kunyakua kitita cha Sh500,000. 

Dodoma. Shindano la kuibua vipaji kwa wanafunzi wa shule za msingi jijini Dodoma nchini Tanzania limehitimishwa leo Jumatano Desemba 4, 2019 kwa shule ya msingi Chadulu kuibuka mshindi na kunyakua kitita cha Sh500,000.

Shindalo hilo lililojulikana kama Mavunde Talent Search 2019 lilianza Novemba 25, 2019 kwa kushirikisha shule 25 zilizokuwa na washiriki 500 kwa ufadhili wa mbunge wa Dodoma Mjini (CCM),  Anthony Mavunde.

Lengo la shindano hilo lilikuwa kuibua vipaji katika mpira wa pete, miguu, uimbaji, kompyuta na uchoraji ambapo wanafunzi walionyesha uwezo mkubwa hasa katika uimbaji.

Shule zilizoibuka na ushindi wa jumla ni Chadulu ikifuatiwa na DCT Bishop Stanley na ushindi wa tatu ulikwenda kwa shule ya msingi Mlimwa.

Akitoa zawadi kwa washindi bora 20, mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Patrobasi Katambi amesema shindano hilo linatoa nafasi nzuri kwa washindi ambao sasa watakwenda kusomeshwa katika shule ya Elen White English Medium  ambayo inakuza vipaji.

"Mbunge wenu amewalipia ada katika shule hiyo na ametoa vifaa vyote muhimu ambavyo vinatakiwa kwa wanafunzi, mbali na zawadi za shule lakini watoto watasimamiwa kikamilifu kwenye taaluma," amesema Katambi.

Katambi amesema wanafunzi hao walijiandaa kikamilifu kiasi cha kuwatoa machozi wazazi na watumishi waliohudhuria tamasha hilo.

Amewaomba walimu kuendelea kuwatia moyo wanafunzi kwani vipaji vinalipa, wazazi hawapaswi kukata tamaa kuwatia moyo wawapo majumbani.