Sitasita kufanya siasa, asema Maalim Seif

Unguja. Licha ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba kumuhoji kwa saa mbili, mshauri mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatasita kufanya siasa na ataendelea na shughuli hizo kama kawaida.

Maalim Seif na Mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa chama hicho, Salim Bimani walitakiwa kufika ofisi za makao makuu ya jeshi ya polisi Wete jana, saa tatu kwa mahojiano.

Baada ya mahojiani akizungumza na Mwananchi Maalim Seif alisema walihojiwa kwa saa mbili na mazungumzo yalijikita kumuhusisha yeye na kufanya mkutano wa hadhara katika Shehia ya Kiuyu, wilaya ya Micheweni, Desemba 9, mwaka jana.

“Mimi na viongozi wenzangu tunashangazwa na madai hayo ya Jeshi la Polisi, kwani hatujawahi kufanya mkutano wa hadhara,” alisema.

Alisema siku hiyo walitembelea na kufanya mazungumzo na baraza mbalimbali za chama kwa lengo la kuimarisha chama kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.

Awali, Mwenyekiti wa kamati ya uhusiano ya chama hicho, Salim Bimani alisema kinachofanywa kwenye siasa za Tanzania hususani Zanzibar kinashangaza.

Alieleza hivi karibuni vijana wa CCM waliandamana maeneo yote ya Unguja bila ya kuulizwa lolote, huku wakichana bendera za chama chao.

Alisema kwa mazingira hayo ni wazi watawala na vyombo vyengine vimeamua kufanya kazi ya kukandamiza upinzani.

Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Sadi Khamis alipoulizwa suala hilo alisema wamelazimika kumuhoji Maalim Seif na msaidizi wake baada ya kupokea maelekezo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Alisema wao kama watendaji na watu wanaohusika kukusanya ushahidi wa makosa mbalimbali, wametekeleza agizo hilo ambalo baada ya kukamilisha watapeleka jalada sehemu husika kwa hatua zaidi za kisheria.

Alieleza kuwa katika upelelezi wao wamegundua watuhumiwa wana kesi ya kujibu, lakini hayo yote yatabainika baada ya kufika hatua nyingine za kisheria.