Magufuli kumalizia Dodoma, Majaliwa Lindi na Mtwara

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Polepole alisema Rais Magufuli kabla ya kumalizia mkoani Dodoma atapitia mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na mwishowe jijini Dodoma mahali aliposema atapiga kura.

Dar es Salaam. Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, John Magufuli kesho ataendelea kujinadi mkoani Pwani kabla ya kuhitimisha kampeni zake mkoani Dodoma, Oktoba 26 ikiwa ni siku mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Wakati huohuo, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa ambaye imeelezwa kuwa yupo Dar es Salaam kwa kazi ya kiserikali, atakwenda Mtwara na Lindi kwa ajili ya kumalizia kampeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Polepole alisema Rais Magufuli kabla ya kumalizia mkoani Dodoma atapitia mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na mwishowe jijini Dodoma mahali aliposema atapiga kura.

Kuhusu Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgombea mwenza na pia Makamu wa Rais, yeye atakwenda Zanzibar Unguja, Pemba na baadaye kumalizia mkoani Morogoro.

Polepole alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wanachama wao kutojihusisha na vurugu ya aina yoyote, akiwaagiza kufanya kampeni za kistaarabu na kuwataka warudi nyumbani baada ya kupiga kura.

Pia Polepele amevitaka vyombo vya dola likiwamo Jeshi la Polisi, Tume ya Uchaguzi (NEC) na ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kuhakikisha kuwa wanalinda amani ya Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu

“Kama kule Zanzibar watu wetu wanakatwa mapanga baada ya mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Act Wazalendo kusimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba; huu si uungwana,”

“Pia kijana wetu wa CCM Dodoma, kijana mdogo wa chuo kikuu wamemteka kumpiga na kupoteza maisha yake na ushahidi upo na mambo yako wazi. Songwe pia wamempiga na kumponda mawe kijana wa CCM na kupoteza maisha sina cha kusema, Polisi zingatieni hili na haki itendeke watuhumiwa wafikishwe Mahakamani,”alisema.

Kikwete amnadi Magufuli

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete jana katika mkutano wa kampeni kuwanadi wagombea ubunge wa Mbagala na Temeke, alieleza sababu za CCM kuendelea kuongoza nchi, akijinasibu kuwa kina sera zinazounganisha Taifa na kujenga umoja, udugu na upendo.

“Nchi yetu ina umoja amani na utuluivu; zipo nchi za wenzetu zinahangaika kuutafuta umoja utulivu na amani kwa sababu ukabila na udini unawatafuna; wanagawanywa kutokana na maeneo wanayotoka,”alisema Kikwete.

Alieleza sababu ya pili ya kuichagua CCM ni kutokana na kutengeneza ilani za uchaguzi zinazotambua changamoto za wananchi.

“Ukisoma ilani za CCM ndani yake kuna mapendekezo yanayoeleza namna ya kuzitatua na CCM imekuwa makini kuhakikisha ilani inatekelezeka,”alisema.

Aidha, Kikwete aliwasihi wananchi kutopoteza miaka mitano kwa kumchagua kiongozi asiye sahihi, huku akisema ajenda ya chama chao mwaka 2015 ilikuwa ni kupambana na rushwa na hivyo walikubaliana kutafuta mgombea asiyekuwa na makandokando.

“Chaguo letu la Magufuli hatukukosea; hata kwenye ilani tuliandika ianzishwe mahakama maalum kwa ajili ya kupambana na rushwa na ndio maana kwenye uchaguzi huu sijamsikia mgombea yoyote akizungumzia masuala ya rushwa..Kazi kubwa imefanyika kwenye nyanja zote na mambo yameenda shwari,’’ alisema.