ACT-Wazalendo nao waomba kujiunga kesi ya ukomo wa urais

Wakili wa ACT- Wazalendo, Jebra Kambole

Muktasari:

  • ACT- Wazalendo nao waenda mahakamani kutetea maslahi yao kuhusu kesi ya ukomo wa urais

Dar es Salaam. Chama cha upinzania nchini Tanzania cha ACT- Wazalendo kimewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania kikiomba kujiunga katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mkulima Dezydelius Patrick Mgoya, akihoji kuwepo kwa kikomo cha urais nchini.

Maombi ya ACT-Wazalendo kujiunga katika kesi hiyo yamebainishwa leo Jumatatu, Septemba 30, 2019 na Jaji Kiongozi wa Tanzania, Dk Eliezer Feleshi wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya maelekezo maalumu ya namna ya usikilizwaji wa pingamizi la awali la Seriali dhidi ya kesi hiyo.

Jaji Kiongozi Dk Feleshi ndiye kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo. Wengine katika kesi hiyo ni Dk Benhajj Masoud na Seif Kulita.

Maombi hayo ya ACT- Wazalendo yamewasilishwa mahakamani hapo na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, inayowakilishwa na kampuni ya uwakili ya Law Guards Advocates chini ya hati ya dharura, wakiomba maombi yao hayo yasikilizwe haraka. 

Kutokana na maombi hayo, Mahakama imesimamisha usikilizwaji wa kesi ya msingi na kuamua kusikiliza kwanza maombi hayo ya ACT-Wazalendo kabla ya kuendelea na shauri la msingi.

“Kwa kuwa pannel (jopo) limefahamishwa kuwepo kwa maombi madogo yanayotokana na shauri la msingi, basi tunalazimika kusimamisha mchakato wa usikilizwaji wa shauri la msingiili kusikiliza kwanza maombi haya,’, amesema Jaji Feleshi.

Amesema maombi hayo ya ACT- Wazalendo yatasikilizwa na Jaji mmoja ambaye ataliarifu jopo hilo kuhusu uamuzi wa maombi hayo na akapanga kesi hiyo kutajwa Oktoba 25,2019 kwa ajili ya maelekezo muhimu.

Wakili wa ACT- Wazalendo, Jebra Kambole amelieleza Mwananchi maombi ya wateja wake  yamepangwa kusikilizwa na Jaji Benhajj na kwamba yamepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza keshokutwa, Jumatano, Oktoba 2, 2019.

Katika maombi hayo, pamoja na mambo mengine, chama hicho kinadai kuwa ikiwa uamuzi wa kesi hiyo utapitishwa bila wao kushirikishwa kitaathirika na kwamba kina haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkulima huyo mkazi wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, Patrick Dezydelius Mgoya amefungua kesi hiyo Mahakama Kuu, Masjala Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya ibara ya katiba inayoweka ukomo huo wa urais.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo namba 19 ya mwaka 2019 Mgoya anahoji Ibara ya 40 (2) ya Katiba ambayo inaweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano (10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.

Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42(2) ya Katiba, kwa kuhusianisha na  masharti ya Ibara za 13, 21 na 22 za Katibahiyo. 

Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.

Katika hati yake ya kiapo kinachounga mkono kesi hiyo, Mgoya anadai kuwa lakini Ibara ya 40(2) ya Katiba inaweka ukomo wa muda wa mtu kuchaguliwa kuwa rais, kwamba mtu hawezi kuchaguli zaidi ya mara mbili kushikilia wadhifa wa urais.

Hivyo anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40(2) yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) za Katiba hiyohiyo kwa kutoa mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais kwa ukomo wa miaka 10 tu.

Mgoya anadai ukomo uliowekwa chini ya Ibara ya 40(2) ya Katiba yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma kwa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na usawa mbele ya sheria  chini ya Ibara ya 21 na 13

Hata hivyo, Serikali imewasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo ikiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali kabla ya kuisikiliza huku ikibainisha sababu nane za pingamizi hilo.

Miongoni mwa hoja hizo za pingamizi, Serikali inadai mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kwamba mwombaji hati ya kiapo inayounga mkono shauri hilo ina kasoro za kisheria zisizoweza kurekebishika, hasa sehemu ya uthibitisho wa taarifa zilizomo.

Serikali pia inadai mwombaji hana haki ya kisheria kufungua na kwamba nafuu anazoziomba mwombaji haziwezi kutolewa kwa kuwa zinakiuka kifungu cha 44 cha Sheria ya Mawakili, Sura ya 341, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.