ATCL kumsafirisha bure anayepumulia mashine

Wednesday September 11 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema lipo tayari kumlipia gharama za usafiri mgonjwa anayepumulia mashine, Hamad Awadh (28) kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mumbai, India ikiwa atapangiwa na madaktari kutibiwa katika mji huo.

Shirika hilo litatoa tiketi mbili za ndege kwenda India na kurudi Tanzania.

Hayo yameelezwa ikiwa zimepita siku tano tangu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuahidi kutoa Sh11.5 milioni, Sh10 milioni zikiwa kwa ajili ya matibabu na Sh1.5 milioni kumsaidia gharama za umeme.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Septemba 10, 2019 mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema watagharamia usafiri wa kwenda na kurudi.

“Tumempatia masharti yetu kwa kuwa ATCL inakwenda Mumbai India, tutamsafirisha iwapo atapata hospitali iliyopo Mumbai ili iwe rahisi kwake katika usafiri kwa maana tutamfikisha pale na tutaweza kumrudisha bila shida yoyote kwa gharama zetu,” amesema Matindi.

Awadh amelieleza Mwananchi kuwa tayari watu mbalimbali wanampigia simu wakitaka kujua gharama za matibabu nje ya nchi, lakini inakuwa vigumu kuzitoa kwani hajafanikiwa kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila kufanyiwa upya vipimo.

Advertisement

“Shirika la Ndege ATCL walinitafuta na wakaniambia gharama za kwenda India na kurudi ni juu yao. Ninapigiwa simu na watu mbalimbali hawataki kujitambulisha lakini wanahitaji tu kujua gharama ili waniwekee benki, wanashindwa kuchangia sababu sijajua gharama halisi.”

"Mloganzila wameniambia niende kufanyiwa uchunguzi upya na jopo la madaktari wangu, lakini nimekwama na sijui itakuwaje mtungi huu (anauonyesha) hauwezi kuingia kwenye gari, sina namna ya kufika, nawaomba wanitumie ambulance (gari la wagonjwa) yenye mtungi mdogo au hospitali yoyote inisaidie niweze kufika,” amesema Awadh.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila, Dk Julieth Magandi amesema kuwa jopo la madaktari limekubaliana kumfanyia uchunguzi upya Awadh ili kujiridhisha kuhusu matibabu yake ya mwendelezo, lakini anatakiwa atafute usafiri mpaka hospitalini hapo.

Kuhusu umeme, Awadh ameomba msaada baada ya kushindwa kumudu gharama za malipo ya nishati hiyo kutokana na mashine anayotumia kumsaidia kupumua kutumia umeme mwingi, hulipia zaidi ya Sh50,000 kwa wiki.

Septemba 5, 2019  Tanesco ilipokea maombi hayo na kumchangia fedha hizo zikiwemo Sh1.5 milioni za kulipa umeme kwa miezi sita.

Septemba 7 na 8, 2019 mafundi wa Tanesco walifunga nishati hiyo na sasa Awadh ameondokana na kulipa gharama za umeme kama awali na kuweza kutumia vifaa vingine kama feni, friji, televisheni na redio.

“Tanesco walikuja Jumamosi iliyopita wakapima, wakarekebisha nyaya juu wakafunga main switch na mita nyingine na Jumamosi nilianza kutumia uniti 210 waliweka kama dharura kwamba watakapokuja wataniwekea umeme wa Sh1.1 milioni  na kila utakapoisha wao wataweka umeme mwingine, bado wananipigia simu wananiuliza maendeleo yangu,” amesema.

Kaimu Meneja Mawasiliano Tanesco, Leila Muhaji amesema baada ya kufunga umeme huo wanatarajia kumkabidhi fedha za matibabu, “Tutamkabidhi hivi karibuni Sh10 milioni tulizoahidi kwa ajili ya matibabu.”

Jirani wa Awadh, Khasim Membe mkazi wa Majumbasita Ukonga, amesema kabla ya kufungiwa umeme huo Awadh alitumia fedha nyingi kiasi cha kushindwa kumudu mahitaji mengine.

“Tanesco kumuwekea umeme ni jambo zuri ambalo wamesaidia kwa kiasi kikubwa lakini tatizo kwa sasa gesi tunaomba msaada zaidi anahitaji maji safi, maziwa tunaomba wajitokeze zaidi ili mpaka anapokwenda kwenye matibabu arudi akiwa mzima ajitegemee yeye na familia yake kama ilivyokuwa mwanzo anatamani maisha yake ya zamani maana hata nje hatoki,” amesema Membe.

SOMA ZAIDI

Advertisement