Adakwa na kilo 150 za bangi

Muktasari:

Polisi wilaya ya Serengeti inamshikilia, Kitende Magabe baada ya kumkuta akijiandaa kusafirisha kilo 150 za bangi.

Serengeti. Polisi wilaya ya Serengeti inamshikilia, Kitende Magabe baada ya kumkuta akijiandaa kusafirisha kilo 150 za bangi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Oktoba 17, 2020 kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa leo katika eneo la shule ya msingi Mapinduzi akisubiri magari ya kuelekea Bunda na Mwanza.

"Alikuwa na magunia mawili ya bangi akijiandaa kusafirisha na sasa mahojiano yanaendelea ili kubaini alitokea wapi na mzigo huo na hatua zaidi zitachukuliwa, "amesema.

Taarifa zilizoifikia Mwananchi Digital zinaeleza kuwa mtuhumiwa anadaiwa kutokea Tarime na kwa kuogopa vizuizi vya polisi katika neo la Kirumi alipitia Serengeti na kwenda kusubiri magari nje ya stendi.

Imeelezwa kuwa polisi walipata taarifa hiyo na kufuatilia ambapo walifanikiwa kumnasa na bangi hiyo ambayo ilikuwa imefungwa ndani ya magunia, kufunikwa na nguo.

"Mtuhumiwa kwa kuwa ni..., inakuwa vigumu kumtilia shaka kwa kuwa tulikuwa na taarifa ilikuwa rahisi kumnasa maana mbinu ya kutumia watu ambao hawatiliwi shaka ndiyo inatumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, " zinaeleza taarifa hizo.