Ali Kiba atoa msaada shule aliyosoma

Muktasari:

Ali Kiba amesema somo la muziki alilofundishwa katika Shule ya Msingi  Upanga ndio limemfanya awe mwanamuziki.

Dar es Salaam.  Ali Kiba amesema somo la muziki alilofundishwa katika Shule ya Msingi  Upanga ndio limemfanya awe mwanamuziki.

Kutokana na kutosahau hilo  leo Jumamosi Septemba 21, 2019, Ali Kiba ameitembelea shule hiyo iliyopo Upanga na kuzindua majengo yaliyokarabatiwa pamoja na eneo maalum la kutupa taka alilolijenga.

Amebainisha kuwa wakati anafundishwa somo hilo alikuwa hajajikita katika muziki lakini kadri siku zilivyozidi kwenda aligundua ana kitu ndani yake kuhusu tasnia hiyo.

"Najielewa ni wapi nilikotoka, nilichofundishwa Upanga ndio kimenisaidia katika maisha yangu. Kulikuwa na somo la muziki wakati nafundishwa nilikuwa naona vitu vina chorwa tu lakini leo ndio kazi muhimu maishani mwangu, "amesema Ali Kiba.

Amesema kupitia muziki amefungua taasisi huku akikumbuka baadhi ya matukio aliyoyafanya shuleni hapo na wenzake, “Kila Ijumaa tulikuwa tunaruhusiwa kwenda msikitini, ila kuna siku tulizuiwa kwa sababu tulikuwa hatujamaliza kazi darasani.”

"Mimi na wenzangu watatu tulipanda juu ya bomba la bendera na kushuka nalo hadi kwenye dirisha na kufanikiwa kutoroka.”

Mwalimu mkuu wa shule hiyo,  Ailika Yahaya amesema Ali Kiba  amewajengea eneo la kutupa taka, huku akiwataka watu wa kada mbalimbali kukumbuka walipotoka.

"Kuna kasumba ya wazazi kuona  watoto wao wakiimba muziki wanapoteza muda na kuwataka wafanye vitu vingine wakiamini ndiyo vina maana. Ninachoamini mtoto anaweza kufanikiwa kwa fani yoyote na akasimama imara," amesema Ailika.