VIDEO: Bei ya mahindi, unga yapaa nchini

Dar/mikoani. Bei ya unga wa mahindi imepanda katika baadhi ya maeneo nchini, lakini waziri wa Kilimo na Ushirika, Japhet Hasunga amesema hakuna uhaba wa chakula ila mahitaji ya soko yameongezeka.

Utafiti uliofanywa na Mwananchi katika maeneo mbalimbali nchini umegundua kuwa bei ya unga imekuwa ikipaa mara kwa mara katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Bei ya unga imegundulika kuwa imepanda kwa kati ya asilimia 20 hadi kufikia 40.

Kilo moja ya unga wa mahindi kwa maeneo mengi inaanzia Sh1500 na Sh1600 kutoka Sh1200 katika maduka na masoko mbalimbali nchini.

Viroba vya unga wa sembe vya kilo tano kwa sasa vimefikia kiasi cha Sh8,000 kutoka Sh6,500 miezi miwili iliyopita katika maeneo kadhaa.

Waandishi wa Mwananchi katika mikoa mbalimbali ikiwamo ile inayojulikana kwa kuuza mahindi kwa wingi kama Dodoma, Ruvuma, Mbeya na Katavi wameripoti kuwa kuna ongezeko la bei katika bidhaa hiyo muhimu.

Mikoa mingine ambayo pia kulifanyika utafiti ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mwanza, Mbeya na Njombe.

Katika mikoa ambayo Mwananchi imefanya utafiti, Mwanza ndio unaoongoza kwa kuwa na bei ya juu ya mahindi wakati Njombe kuna bei ya chini zaidi.

Wadau wa biashara ya unga wametoa sababu mbalimbali ambazo zimesababisha ongezeko hilo la bei.

Serikali kwa upande wake imeelezea hali hiyo kuwa imechangiwa na mahitaji na uzalishaji wa unga baada ya kuruhusu wakulima kuuza nje zao hilo.

Akizungumzia suala hilo, Waziri Hasunga amesema uamuzi wa Serikali wa kufungua milango kwa wakulima kuuza mahindi nje ya nchi umesababisha kuwepo kwa mahitaji makubwa.

Ruvuma

Mkoa wa Ruvuma unajulikana kama miongoni mwa mikoa ya Tanzania inayozalisha mahindi kwa wingi.

Bei ya mahindi mkoani Ruvuma imepanda kutoka Sh45,000 hadi Sh 67,000 kwa gunia la kilo 100 huku kilo moja ya mahindi ikiuzwa kati ya Sh630 hadi Sh670 .

Bei ya unga wa mahindi nayo imepaa kutoka Sh1000 kwa kilo na kufikia Sh1500.

Akizungumza na Mwananchi jana, mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mazao (Uwamaviru), Eusebius Wella alisema bei hizo zimepanda kutokana na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kufuata mahindi huko.

Mbeya

Katika Jiji la Mbeya kilo moja ya unga wa mahindi inauzwa kati ya Sh1,400 mpaka Sh1,500 wakati awali miezi kama hii ilikuwa inauzwa kwa kilo kwa bei ya Sh900 mpaka Sh1,000.

Mfanyabishara wa duka la jumla, Hashim Mohammed wa Forest jijini Mbeya alisema awali walikuwa wakiuza kwa ujazo wa kilo tano kwa bei ya Sh6,000 lakini ni wiki mbili sasa umepanda hadi kufikia Sh7,500.

Dodoma

Soko la kimataifa la Kibaigwa lililopo mkoani Dodoma ndio linasifika nchini kwa kuuza mahindi kwa wingi.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwa bei ya mahindi imepanda na kufikia Sh820 kwa kilo, lakini wafanyabiashara wanasema bado iko chini ukilinganisha na bei ya Sh1,350 kwa msimu kama huu mwaka 2016.

Wafanyabiashara hao wanadai kuwa miezi hii ya Novemba bei hushuka na kuwa kati ya Sh 540 hadi Sh700 kwa kilo.

Wafanyabiashara wa mahindi ndani ya soko hilo wanalia uhaba wa mahindi kwamba ndiyo sababu ya kupanda kwa bei.

Mahindi mengi zaidi katika soko hilo hutokea Kiteto na maeneo mengine ni Kilindi, Mpwapwa na Kongwa, lakini uhaba umesababishwa na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali nchini kufuata mahindi.

Kilimanjaro

Katika mji wa Moshi, bei ya gunia la mahindi la kilo 100 imepanda kutoka Sh85,000 hadi Sh95,000 wakati bei ya unga wa mahindi ikipanda kutoka Sh28,000 hadi Sh30,000 kwa mfuko wa kilo 25.

Wafanyabashara katika soko la Juu na soko la Mbuyuni mjini Moshi walilieleza Mwananchi kuwa bei ya mahindi itaendelea kupanda kutokana na wakulima wengi kutopata mavuno msimu huu.

Mwanza

Mwanza ndio mkoa unaoongoza nchini kwa bei ya mahindi kuwa juu kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Kilimo na Ushirika.

Jijini Mwanza, debe la mahindi lililokuwa likiuzwa kati ya Sh18,000 na Sh20,000 sasa linauzwa Sh25,000 na gunia limepanda kutoka Sh80,000 na kufikia kati ya Sh115,000, Sh120,000 na Sh130,000.

Arusha

Hali iko hivyohivyo katika mikoa mbalimbali ambapo kwa mkoa wa Arusha, kilo moja ya unga wa sembe imepanda kutoka Sh1,000 mwezi Januari hadi kufikia Sh1,400 kwa kilo mwezi Novemba.

Morogoro

Mkoani Morogoro, bei ya Mahindi gunia moja la debe saba limepanda kutoka Sh75,000 hadi kufikia kati ya Sh105,000 na Sh107,000 na kuna uwezekano mkubwa wa bei hizo kupanda zaidi.

Wafanyabiashara wa Morogoro wametaja sababu ya kupanda kwa bei kuwa ni kutokana na wakulima kupata fursa kuuza mahindi kwa wafanyabiashara wa nje.

Njombe

Mkoa wa Njombe umetajwa kuwa ndio wenye bei ya chini ya mahindi, kwani gunia la mahindi la kilo 10 linauzwa kati ya Sh50,000 hadi Sh55,000.

Tamko la Serikali

Waziri Hasunga alisema kupanda kwa bei sio maana yake kuwa kuna uhaba wa chakula, kwani kilichosababisha ni mahitaji ya soko.

Hasunga alisema baada ya Serikali kuruhusu wakulima kuuza ina maana wamepata fursa kwa kuwepo mahitaji makubwa sokoni1 ingawa kwa kiasi kikubwa anafahamu wananchi wameathirika.

“Wakulima wetu kwa muda mrefu wamekuwa wanahangaika kupata soko, sasa wananufaika nadhani dawa ni kuongeza uzalishaji wa mahindi,” alisema Hasunga.

Hali ya chakula nchini

Tovuti ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaonyesha walikuwa na akiba ya chakula ya tani 61,710 kwa mwezi Septemba, mwaka huu.

Kunaonyesha upungufu ukilinganisha na kufikia Septemba, mwaka jana ambapo mfuko huo ulikuwa umehifadhi chakula cha tani 78,224.

Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuhusu bei za vyakula inaonyesha bei ya kilo 100 za mahindi ilikuwa imefikia Sh71,046 mwezi Septemba, mwaka huu tofauti na Sh 39,691, ambayo ilikuwa bei ya kilo 100 Septemba mwaka jana.

‘Unga watinga bungeni’

Mbunge wa Mtambile (CUF) Masoud Abdallah Salim alizungumzia suala la bei ya unga kupanda wakati akichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo jana.

Salim alilalamikia kupanda kwa bei ya chakula, akisema mwaka 2011 bei ya debe moja la mahindi ilikuwa kati ya Sh5,000 hadi Sh6,000 lakini mwaka 2017 ilipanda na kufikia Sh12,000 na sasa imefika Sh18,000 na kuendelea.

“Kilo moja ya unga wa sembe ilikuwa inauzwa kati ya Sh700 hadi Sh1000 siku za nyuma. Leo kilo ya sembe imefika Sh1,500,” alisema mbunge huyo.