Binti adaiwa kumuua mpenzi wake wa miaka 50

Friday January 17 2020

 

By Stella Ibengwe, Mwananchi [email protected]

Shinyanga. John Maguzu (50), mkazi wa mtaa wa Majengo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga nchini Tanzania ameuawa kwa kupigwa na tofali kichwani na mpenzi wake wa kike aliyefahamika kwa jina moja la Aneth (22).

Habari zilizopatikana kutoka wilayani Kahama na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Joseph Paul zimeeleza tukio hilo lilitokea saa 2:00 usiku wa Januari 16, 2020.

“Polisi inamshikilia binti anayetuhumiwa kuhusika na tukio hilo kwa mahojiano na uchunguzi zaidi,” amesema Kaimu Kamanda huyo

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa wa Majengo, John Samuel amesema mauaji hayo yalitokea na ugomvi uliotokana na marehemu kumhoji mpenzi wake kwa nini ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.

“Baada ya swali hili, wapenzi hao walikuwa na mvutano ndipo msichana yule anadaiwa kuchukua tofali na kumponda nayo kichwani mpenzi wake wa kiume,” amesema Samuel

Amesema watu waliokuwepo eneo hilo walimkimbiza marehemu John katika zahanati jirani ya Bakwata kabla ya kwenda naye polisi kwa ajili ya kupatiwa fomu namba tatu (PF3) na kumkimbiza hospitali ya Halmashauri ya Nji Kahama ambako mauti yalimkuta akiwa mapokezi.

Advertisement

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama, Dk George Masasi amesema uchunguzi wa awali wa kitabibu umebaini kuwa ubongo wa marehemu ulipata hitilafu uliosababishwa na kuumizwa kwa fuvu la kichwa.

Advertisement