Bunge la Tanzania laanza mchakato wa kutumia Kiswahili

Tuesday April 2 2019

 

By Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha lugha ya Kiswahili inatumika katika shughuli zote bungeni ili kuikuza lugha hiyo ya Taifa.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo jana Jumatatu Aprili mosi 2019 wakati akizindua matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Amesema kwa sasa shughuli za Bunge zinafanyika kwa lugha ya Kiswahili isipokuwa baadhi ya miswada ambayo ipo kwa lugha ya Kiingereza licha ya kujadiliwa kwa lugha ya taifa.

“Tunataka kuhakikisha hata hiyo baadhi ya miswada ambayo ipo kwa lugha ya Kiingereza inakuwa kwa lugha ya Kiswahili na wapo wabunge wengine wanatumia ‘kiswakinge’ (Kiswahili na Kiingereza) lakini hilo litaisha kwani tutataka kuitangaza lugha yetu,” amesema Ndugai

Kiongozi huyo wa Bunge alilipongeza shirika la BBC kwa kutambua umuhimu wa kuwafikia wana Dodoma na Watanzania kwa kufanya uzinduzi wa matangazo yao katika mkoa huo, huku akiwataka kuendelea na kasi waliyonayo ya kukuza lugha ya Kiswahili.

Naye mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Odhiambo Joseph alisema lengo la kufanya uzinduzi huo Dodoma ni kuunga mkono juhudi za Serikali kuhamia makao makuu ya nchi.

Advertisement

“Tanzania tuna wasikilizaji milioni 12 hivyo watarajie mambo mazuri kutoka kwetu na niwaambie kuwa kule Dar es Salaam tutabaki na bureau (kitengo) lakini matangazo yatarushwa kutoka hapa Dodoma,” amesema Odhiambo.

Kwa upande wake, kaimu makamu mkuu wa chuo Udom, Profesa Donald Mpanduji  amesema chuo hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa kukuza lugha ya Kiswahili kwani ni cha kwanza Tanzania kutoa shahada ya Kiswahili.


Advertisement