Dk Omary Nundu alitoa neno msamaha wa Magufuli kwa Nape saa chache kabla ya kufariki

Thursday September 12 2019Dk Omary Nundu

Dk Omary Nundu 

By Burhani Yakub, Mwananchi byakub @mwananchi. co. tz

Tanga. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe amesema saa chache kabla Dk Omary Nundu kufariki dunia alimtumia ujumbe uliompongeza Rais John Magufuli kumsamehe mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.

Dk Nundu, mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania alifariki dunia jana Jumatano Septemba 11, 2019.

Mwambe ameeleza hayo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 wakati akitoa salamu za rambirambi za kituo hicho katika mazishi ya Dk Nundu, nyumbani kwake Mwakidila mjini Tanga.

Amesema usiku wa kuamkia jana Septemba 11, 2019, alitumiwa ujumbe na Dk Nundu aliyempongeza  kiongozi mkuu huyo wa nchi kumsamehe Nape.

"Masikini kumbe alikuwa akiniaga kwa mtindo huo. Nitamkumbuka kwa ushauri aliokuwa akinipa katika kukiendeleza kituo na Taifa kwa ujumla,” amesema Mwambe.

Septemba 10, 2019 Nape alikwenda Ikulu kumuomba msamaha Magufuli kufuatia kuhusishwa na sauti zilizosambaa mitandaoni zikizungumzia barua ya makatibu wa zamani wa CCM na pia hali ya chama kudhoofika na kumkejeli kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Advertisement

Wabunge wengine waliomuomba msamaha Magufuli ni William Ngeleja (Sengerema) na January Makamba (Bumbuli).

Mwili wa Dk Nundu umezikwa leo saa 10 jioni katika makaburi ya Mwakidila.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye aliongoza ujumbe wa Serikali katika mazishi hayo, kubainisha kuwa nchi imempoteza kiongozi aliyeweka mbele maslahi ya Taifa na kuichukia rushwa kwa vitendo.

 

Advertisement