VIDEO: Jafo akiri kasoro uchukuaji fomu uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Seleman Jafo amekiri siku ya kwanza ya kuchukua fomu za uchaguzi wa Serikali za mitaa kutokwenda vizuri, kuwataka watendaji kujirekebisha.


Dodoma. Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Seleman Jafo amekiri siku ya kwanza ya kuchukua fomu za uchaguzi wa Serikali za mitaa kutokwenda vizuri, kuwataka watendaji kujirekebisha.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 30, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Dodoma ikiwa ni siku moja tangu wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa kuanza kuchukua fomu.

Kauli hiyo imekuja huku chama cha Chadema kikimuandikia barua kueleza malalamiko yake katika maeneo tisa kuhusu uchaguzi huo.

Leo Jafo amesema yametolewa malalamiko katika kata 72 nchini na tayari timu ya uchaguzi ya Tamisemi inayashughulikia huku akizitaka kamati za rufaa za Wilaya  kufanya kazi hiyo.

Mapema leo Chama cha Wananchi (CUF) kilizungumza na waandishi wa habari na kueleza ukiukwaji wa masuala mbalimbali katika baadhi ya maeneo, ikiwa ni pamoja na wagombea wa upinzani kunyimwa fomu na wengine kukamatwa na kuwekwa rumande.

Baadhi  maeneo yaliyotajwa na CUF  ni Wilaya ya Liwale wakidai kuwa wagombea wake na vyama vingine vya upinzani hawakupewa fomu  huku wale wa CCM wakipelekewa fomu hizo majumbani mwao.

"Ni kweli huko Liwale tumesikia kuna shida, tumetoa maelekezo ya nini kifanyike ili kuondoa hali hiyo, uchaguzi huu ni wa upendo tunapaswa kupendana wote," amesema Jafo.