Japan yaipiga jeki KCMC magari ya wagonjwa

Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi, Gabriel Chisseo akito amaelezo ya magari mawili ya kisasa ya kubebea wagonjwa yaliyotolewa kwa hospitali hiyo na ubalozi wa Japan nchini Tanzania

Muktasari:

Magari hayo mawili ya kubeba wagonjwa yaliyotolewa na ubalozi wa Japan nchini Tanzania ni ya kisasa katika daraja la juu la magari ya kubebea wagonjwa wa dharura.

Moshi. Hospitali ya rufaa ya KCMC imepokea magari mawili yenye vifaa vya kisasa ya kubebea wagonjwa kutoka ubalozi wa Japan nchini Tanzania.

Baada ya kupokea magari hayo leo Oktoba 17, hospitali hiyo inayomilikiwa na Shirika la Msamariamwema (GSF), ililitoa moja kwenda kituo cha afya cha Serikali cha Pasua.

Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Gileard Masenga amesema wamelitoa gari hilo kutokana na uhusiano mzuri walionayo na Serikali.

“Kutokana na ushirika tulionao na Serikali tuliamua gari moja litumike kituo cha afya Pasua kusaidia wagonjwa watakaohitaji kupelekwa hospitali ya Mawenzi au KCMC haraka,” amesema.

Dk Masenga ambaye ni katibu mtendaji wa GSF, amesema magari hayo yenye thamani ya Sh110 milioni yalipatikana kutokana na andiko waliloliwasilisha kwa Serikali ya Japan kupitia ubalozi wao uliopo jijini Dar es Salaam.

Awali, ofisa uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alisema magari hayo yana vifaa vya kisasa vya huduma za dharura na kupatikana kwake kunaifanya KCMC kuwana magari matano ya kubebea wagonjwa.