Kauli ya Lema kuhusu Gambo yamuibua RPC Shana

Monday February 17 2020

 

By Filbert Rweyemamu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Kauli ya mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kupinga kitendo cha mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Mrisho Gambo kutaka wanaosambaza picha zinazoonyesha barabara za kwenye hifadhi zilivyoharibika kukamatwa, kimewaibua polisi waliomtaka akae mbali na suala hilo.

Juzi Gambo alitembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuwaonya waongoza watalii wanaopiga picha zinazoonyesha ubovu wa barabara, akibainisha kuwa kitendo hicho si uzalendo na kuagiza polisi kuwasaka na kuwakamata.

Leo Jumatatu Februari 17, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amemuonya Lema kukaa mbali na suala hilo.

Shana ameeleza hayo ofisini kwake wakati akifafanua  kufafanua maagizo ya Gambo kwamba ni halali kuyatekeleza kwa sababu waliofanya kitendo hicho wana nia ya kuchafua taswira ya nchi kimataifa.

“Nimeona Lema anasema atashangaa kuona watu wakikamatwa  kwa uchochezi, natumia fursa hii kumtahadharisha  akae mbali na suala hili wakati huu ambao  polisi wenye weledi  wa hali ya juu wakiwa kazini  kuhakikisha mkoa unaendelea salama na utalii unashamiri.”

“Namshauri Lema asikariri  na asome alama za nyakati maana hii sio awamu ya mchezo, kwa pamoja tunaweza, uzalendo wetu kwanza na siasa baadaye,” amesema Shana.

Advertisement

Kamanda huyo wa polisi amesema utalii unachangia asilimia 17.5 ya pato lote la Taifa wakati fedha za kigeni asilimia 25 zinatokana na sekta hiyo huku Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mapato yake kwa mwaka yakiwa Sh143 bilioni wakati Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) likikusanya Sh282 bilioni.

Amesema wakati Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ikitoa gawio la Sh23.5 bilioni serikalini, Tanapa ilitoa gawio  la Sh42.4 bilioni.

Advertisement