Kesi madai ya talaka ya DC yakwama kuendelea

Muktasari:

  • Kesi ya madai ya talaka iliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea baada ya mzee wa baraza mmoja kati ya wawili wanaosikiliza kesi hiyo kufiwa hivyo kuahirishwa hadi Agosti 27,2019.

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea kuisikiliza kesi ya madai ya talaka namba 181 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga kwa kuwa mzee mmoja wa baraza la wazee wanaoshiriki kusikiliza kesi hiyo kufiwa.

Kufuatia hali hiyo, Hakimu anayeisikiliza kesi hiyo, Christina Luguru ameiahirisha kesi leo  Jumatatu Agosti 19,2019 hadi Agosti 27, 2019 ambapo itaendelea kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, Odunga alifungua dhidi ya ndoa yake ya Kikristu  ambayo aliifunga na  Medilina Mbuwuli ambayo ilifanikiwa kupata mtoto wa kike ambaye kwa sasa anasoma kidato cha sita.

Kwenye kesi hiyo, Medilina Mbuwuli ambaye ni mke wa ndoa ya Kanisani wa mkuu huyo wa wilaya Odunga anadai mumewe hajawahi kutoa matunzo ya mtoto wao wa kike mwenye umri wa miaka 18 tangu akiwa chekechea hadi sasa yupo kidato cha sita.

Hata hivyo, alieleza licha ya mumewe kutotoa matunzo hayo, hayupo tayari kupewa talaka kwa sababu ndoa yao ni takatifu ya kanisani na kwamba bado anampenda mume wake na anajua hizo ni changamoto tu zimempitia.

Katika kesi hiyo, Mbuwuli alieleza yeye na mumewe tangu wafunge ndoa mwaka 1998 na kupata cheti cha ndoa  A no 00140917 hawajawahi kuchuma mali yoyote na hana mgogoro na kwamba Odunga amechuma mali na kahaba wa nje ya ndoa.

Hata hivyo alidai  katika ndoa yao Odunga amekuwa akikaa kwake akiwa hana pesa na akipata pesa anaishi kwa mwanamke huyo wa nje ya ndoa na kwamba ana mashahidi wa kutosha.

Aliongeza mumewe ana tabia ya kwenda kwake kila Julai muda ambao hata serikali haina pesa.

Kuhusu mtoto Mbuwuli aliomba mahakama iamuru Odunga amlipe gharama alizotumia kumtunza mtoto wao huyo wa kike mwenye umri wa miaka 18 tangu akiwa chekechea hadi alipo sasa kidato cha sita na kwamba risiti ambazo zinaonesha gharama za ada alizotumia anazo.

Pia ameiomba mahakama iamuru Odunga amuhudumie yeye kama mke  na mtoto wao.

Kwa upande wake, Odunga ambaye ni mdai katika kesi hiyo alidai kuwa Mbuwuli ni mke wake wa ndoa ya Kikristu na kwamba walitengana rasmi mwaka 2003.

Alidai wana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 18 sasa ambaye anaishi na mama yake na hakuna mali yoyote waliyochuma.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi ya kesi nyingine ya DC huyo aliyoifungua mahakamani hapo dhidi aliyefunga naye ndoa ya kiserikali anayeomba mahakama imruhusu kutoa talaka