Kesi ya Shamimu na mumewe, Mahakama inasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu

Muktasari:

  • Kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019 inayowakabili Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida(45) na mkewe, Shamim Mwasha(41) iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania, imeshindwa kuendelea baada ya upande wa mashtaka kudai unasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha(41) umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania wanasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Nsembo na Shamimu wakabiliwa na  shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin, kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,

Wakili wa Serikali ya Tanzania, Wankyo Simon ameieleza Mahakama leo Jumatatu Juni 24, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

 

Simon ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka tunasubiri majibu ya kielelezo kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Simon.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 8, 2019 itakapotajwa na washtakiwa  wamerudishwa rumande.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

 

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha  dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gram 232.70, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, Jijini Dar Es Salaam.

Kwa mara  ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Mei 13, 2019.