Lissu ahutubia mkutano mkuu Chadema akiwa Ubelgiji, atamani kurudi Tanzania

Wednesday December 18 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu ameuhutubia mkutano mkuu wa chama hicho unaoendelea katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam akisema mpango wa kukiua chama hicho iliyopangwa imeshindikana na zaidi imekiimarisha zaidi.

Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa jijini Dodoma na kupelekwa kutibiwa Nairobi nchini Kenya na baadaye nchini Ubelgiji, amedai kulikuwa na mpango wa kuua mfumo wa vyama vingi uliopangwa Februari 6 mwaka 2016.

“Yote yaliyotokea mpaka leo ni utekelezaji wa adhima hiyo ya kuua mfumo wa vyama vingi. Kwa ushahidi huu wa mkutano na mfumo wa uchaguzi katika chama mpaka siku ya leo, hicho walichokidhamiria hakijafanikiwa mpaka leo,” amesema Lissu leo Jumatano Desemba 18,2019

Akizungumza moja kwa moja akitumia ‘video call’ ya WhatApp kutoka Ubelgiji amesema, “baada ya mateso yote tuliyopata, baada ya bonde la uvuli wa mauti, njia iliyobaki ni kuchukua nchi mwaka ujao. Hakuna walichobakiza, watufunga, wametujeruhi na kila mateso, leo tuna nguvu zaidi kuliko tulivyokuwa.”

Amewataka wana Chadema kufanya maandalizi ya kutosha ili ngwe iliyobaki aliyosema siyo ndefu na itakuwa ili wairudishe nchi katika utu, demokrasia na haki binadamu.

Kuhusu afya yake, amesema madaktari wake wamesema nimepona na yuko tayari kurudi nchini.

Advertisement

“Nipo tayari kurudi nyumbani kuungana na makamanda wengine ili tutengeneze nchi. Naombeni tushirikiane ili niweze kurudi nyumbani haraka na salama. Mbele ni kuzuri kuliko huko tulikotoka,” amesema.

Advertisement