Madiwani waliohamia CCM wazua hofu

Saturday January 18 2020

 

By Burhani Yakub,Mwananchi [email protected]

Tanga.Madiwani nane wa CUF katika halmashauri ya Jiji la Tanga waliohamia CCM wamezua hofu kwa baadhi ya makada waliokuwa wamejipanga kuwania katika kata zao.

Baraza la halmashauri hiyo kwa sasa limebaki na madiwani 20 wa CCM na CUF ikiwa na madiwani saba, hivyo kubadilisha sura iliyokuwepo baada ya uchaguzi mkuu 2015 ambapo CUF ilikuwa na madiwani 20, huku CCM ikiwa na madiwani 17.

Akizungumzia hatua hiyo jana, kada wa CCM alisema kitendo cha madiwani hao kinaweza kusababisha mpasuko ndani ya chama hicho.

“Kuhamia kwa madiwani hawa wa CUF kunaweza kuleta mpasuko ndani ya CCM kwa sababu wapo makada walioweka nia ya kuwania kata hizo hasa ikizingatiwa CUF imepunguzwa makali Tanga baada ya Maalim Seif kuhamia ACT –Wazalendo,” alisema Dk Muzzamil Kalokola.

Dk Kalokola ambaye aliingia katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, alisema ni lazima kuwe na muda wa kuwaangalia wanaohamia CCM kwa sababu wengi wamekimbilia huko kwa lengo la kupata madaraka.

Naye Rashid Jumbe ambaye kwa sasa ni kiongoziwa chama cha ACT-Wazalendo alisema si tatizo madiwani hao kuhama, bali wakiendelea kushiriki vikao vya baraza la madiwani kama ilivyokuwa siku za nyuma litakuwa tatizo kubwa.

Advertisement

“Unapohamia chama kingine unapoteza nyadhifa ulizokuwa nayo, hivyo hata hao wameshapoteza sifa ya kuwa madiwani,” alisema.

Advertisement