VIDEO: Magufuli amwagia sifa bosi TCAA, asema angekuwa na binti angemuozesha
Muktasari:
Rais wa Tanzania John Magufuli amemwagia sifa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Anga Tanzania (TCCA), Hamza Johari kutokana na kufanikisha kwake mradi wa ufungaji wa rada katika viwanja viwili vya ndege nchini
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Magufuli amemwagia sifa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Anga Tanzania (TCCA), Hamza Johari kutokana na kufanikisha kwake mradi wa ufungaji wa rada katika viwanja viwili vya ndege nchini.
Navyo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JINA) na Kilimanjaro (Kia). Songwe na Mwanza utekelezaji unaendelea.
“Safi sana hii ndio mifano ya vijana wanaojituma. Sina zawadi ya kukupa lakini mwaka huu (2019) ukiamua kwenda Hijja nitakulipia ili ukamshukuru Mungu kwa utendaji wako,”
““Johari oyee. Kwa kweli wewe ni Johari kweli nasema kwa dhati bila unafiki nilifuatilia utendaji wake wa kazi yupo vizuri. Unamuona mtu anazungumza pointi ningekuwa na binti ningekupa ukaoa,” amesema Rais Magufuli.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 16, 2019 katika hafla ya uzinduzi wa rada za kuongoza ndege katika uwanja wa JNIA.
“Aprili 2019 tulikutana hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa radi nne, leo tumekutana kwa ajili ya kuzindua radi iliyosimikwa hapa JNAI. Nimefurahi sana, wote mnajua mimi sipendi miradi inayoishia njiani hasa ninayoiwekea jiwe la msingi. baadaye unaambiwa haujakamilika,” amesema Magufuli.
Rais Magufuli amewashukuru wabunge kwa kupitisha bajeti kwa ajili ya mchakato huo huku kuwataka waendelee kuchapa kazi.