VIDEO: Magufuli awatosa waziri Lugola, Andengeye

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias  Andengenye hawafai kuendelea na nyadhifa zao kutokana na mambo waliyoyafanya.

 Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias  Andengenye hawafai kuendelea na nyadhifa zao kutokana na mambo waliyoyafanya.

“Nitaendelea kuwapenda lakini kwenye nafasi zenu hapana. Watanzania mmenichagua kusimamia haki na utendaji kazi ndani ya Serikali ili kila fedha ya Watanzania iktumike kwa mujibu wa sheria,” amesema Rais Magufuli.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 23, 2020 katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za Jeshi la Magereza Ukonga, jijini  Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa tume nyingi zimeundwa kuchunguza miradi ya hovyo inayosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Magufuli amesema kutokana na sakata hilo katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu ameandika  barua ya kujiuzulu na amemkubalia.

“Watu wamekosa uadilifu, hivi karibuni kulikuwa na mkataba mmoja wa ajabu unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya  zaidi ya Sh1 trilioni. Mradi huo umesainiwa na kamishna jenerali wa Zimamoto.”

“Haujapangwa kwenye bajeti na haujapitishwa na Bunge. Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wote wa Tanzania waliokuwa wanakwenda katika majadiliano na kulipwa Dola 800 za posho ya vikao,” amesema Magufuli, na kubainisha kuwa hata tiketi za ndege walilipiwa.

Amesema mkataba huo ni wa hovyo kwa sababu ili kuuvunja yaliyoanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa.

“Lugola nampenda sana ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema Sekondari pamoja na mwili na ukubwa wake lakini katika hili hapana. Nilitegemea hata hapa sitamkuta, nasema kwa dhati.”

“Andengenye nampenda sana, ni mchapakazi lakini kwenye hili hapana, nilitegemea asiwepo hapa. Hatuwezi kuendesha nchi kwa misingi ya ajabu namna hii. Yanayokwenda kununuliwa katika mkataba ni ya hovyo.”

Ameongeza, “nampongeza Kingu kwa kuwajibika na hii imempa heshima kwamba angalau ametambua, inawezekana haya hakuyafanya yeye lakini kwa kuwa yeye ni katibu mkuu amewajibika kwa hilo, nampongeza na nitaendelea kumheshimu.”

Magufuli ameshangazwa mtu kusaini Sh1 trilioni wakati jukumu la kukopa fedha ni la Wizara ya Fedha.

Amesema haiwezekani watendaji kufanya mambo wanavyotaka kwa kuwa wataipeleka nchi kubaya na kukiuka misingi na ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Huo ndio ukweli na siku zote nitasimamia ukweli, Ndugu zangu ninajua hili…, wapo pia ofisi ya mwanasheria mkuu, walisubiri mwanasheria mkuu alipofiwa na mke wake wakaenda wakapitisha na kuandika kwa niaba na kwa niaba, wapo nao wanahusika.”

“Wapo wanaohusika katika wizara ya Mambo ya Ndani lakini kitendo cha Zimamoto na ni wasaidizi wa Andengenye ni lazima wajitathmini,” amesema Magufuli