Magufuli azungumzia tena ukomo wa urais

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaeleza wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba muda wa miaka kumi ya uongozi wake utakapomalizika, ataondoka madarakani.

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kazi ya urais ni ngumu na ataondoka madarakani baada ya muda wake wa uongozi kumalizika.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 13, 2019 wakati akiongoza mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika jijini Mwanza.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imesema, “licha ya hamasa kubwa waliyokuwa nayo wajumbe wa halmashauri kuu kutokana na kazi nzuri ya Serikali ya CCM, Magufuli amesisitiza kazi ya urais ni ngumu sana na yeye ataheshimu utamaduni na desturi za CCM, kanuni, katiba ya CCM na Katiba ya nchi na kwamba CCM ni kiwanda cha kuzalisha viongozi na kwa utaratibu ambao chama kimejiwekea kitampata mtu bora zaidi atakayepokea uongozi baada yake.”

Rais Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015 ungwe ya kwanza ya miaka mitano itamalizika mwaka 2020 na ya pili ataihitimisha mwaka 2025 iwapo atachaguliwa tena katika uchaguzi mkuu 2020.

Msimamo huo wa Rais Magufuli ameutoa ikiwa ni siku moja imepita tangu Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Mizengo Pinda kueleza matamanio yake kuona Rais Magufuli anaongezewa miaka mingine mitano baada ya kumaliza muda wake wa uongozi wa miaka 10.

Pinda aliyekuwa waziri mkuu mwaka 2008 hadi 2015 alitoa kauli hiyo jana  Alhamisi Desemba 12, 2019 katika ufunguzi wa semina ya wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM unaofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Mwanza.

Aprili 3, 2019 Rais Magufuli alisema muda wake wa uongozi ukiisha ataondoka madarakani tarehe hiyohiyo kwa kuwa yeye sio rais wa maisha. Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Newala akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Mtwara.

“Mimi napata matumaini makubwa sana kwamba miaka hii kumi uliyopewa itatupeleka pazuri sana, ni kwa kuwa tu katiba zenyewe kidogo ziko tight lakini kama si kwa sababu hiyo  wallah ningesema mzee piga mingine tena ongeza kama mitano tu.”

“Sasa najua hata mkijaribu kumlazimisha atawakatalia tu, lakini nataka niseme kwa namna ninavyoguswa na kazi kubwa unayoifanya,” alisema Pinda.