Majaliwa amtaka bosi TBA ajitathimini, awasimamisha kazi wakurugenzi watatu

Monday November 18 2019

 

By Khadija Mussa, Ofisi ya Waziri Mkuu

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),  Daud Kondoro ajitathmini kuhusu utendaji kazi wake huku akiwasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa wakala huo.

“TBA tunaihitaji lakini watu wake wana shida. Hatuwezi kuwaacha, TBA wasipewe miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni taasisi ya Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya hovyo,” amesema Majaliwa

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi wakurugenzi hao leo Jumatatu, Novemba 18, 2019 wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC eneo la Njedengwa jijini Dodoma.

Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi,  Humphrey Killo, Kaimu Meneja wa Miradi, Abdallah Awadh na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri,  Hamis Kileo.

Majaliwa amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali ukiwemo ujenzi wa jengo la NEC ambalo ujenzi wake ulianza Julai, 2017 na ulitakiwa ukamilike Juni 2018 kwa gharama ya Sh13 bilioni.

Hata hivyo, mradi huo bado haujakamilika na ujenzi wake umesimama.

Advertisement

Akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa ofisi ya NEC, Majaliwa alihoji sababu za mradi huo kutokamilika kwa wakati ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Ujenzi, Humphrey Killo alisema jengo hilo limeshindwa kukamilika kwa sababu wakati walipokuwa wanaanza kazi walibaini kuna vitu vilisahaulika wakati wa uandaaji wa Bill of Quantities(BOQ). TBA ndio waandaaji wa ramani ya jengo hilo na ndio wajenzi.

“Bajeti ya awali ilikuwa Sh10 bilioni wakati wa uandaaji wa michoro ya ujenzi gharama ziliongezeka na kufikia Sh13 bilioni  ambazo ndizo tulikubaliana katika mkataba. Wakati tunaendelea na kazi tuligundua kuna vitu vimesahaulika kwenye BOQ jambo lililoongeza bajeti ya ujenzi na kufikia Sh32 bilioni” Amesema  Killo.

Waziri Mkuu akahoji tena “kutoka Sh13 bilioni hadi kufikia Sh32 bilioni je unaona inakuja vizuri hiyo, Sh10 bilioni hadi Sh13 bilioni tena hadi Sh32 bilioni 32 inazungumzikaje hii na je mwenye jengo mlikubaliana naye? Awali mwenye mahitaji alisema ana Sh10 bilioni  sasa imefikaje 32 je mlimshauri muhusika kuhusu ongezeko hili?

Killo alipotakiwa kueleza sababu za kuongezeka kwa gharama za ujenzi huo amesema waligundua tofauti wakati wakiwa kwenye eneo la ujenzi kwamba kuna kazi zilitakiwa zifanyike lakini katika mkataba hazipo na hawakuwasiliana na muhusika.

Miongoni mwa vitu vilivyosahaulika katika BOQ ya mradi huo ni pamoja na kutokuwepo kwa ghorofa ya nne katika jengo moja wanalolijenga katika mradi huo ambalo ni la ghorofa nane, pia hapakuwa na paa la jengo la kuhifadhia vifaa mbalimbali vya NEC.

Waziri Mkuu amesema miradi mingi inayojengwa na TBA katika maeneo mbalimbali imeshindwa kukamilika kwa wakati, hivyo amemwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama asitishe mkataba huo wa ujenzi na atafutwe mkandarasi mwingine aje amalizie.

“Jengo la Tamisemi lililopo katika mji wa Serikali limejengwa kwa gharama ya Sh1.7 bilioni, nyie wataalamu gani na kwa nini tuendelee kuwaacha ndani ya taasisi? TBA hamfanyi kazi vizuri wakuu wa mikoa na wilaya wanalalamika majengo hayakamiliki ni Serikali gani itakayowavumilia, mmeshindwa kutambua majukumu yenu.”

Waziri Mkuu ameagiza mkandarasi atakayepatikana ahakikishe mradi wa ujenzi huo unakamilika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa na lijengwe kwa kutumia mfumo wa force account.

Advertisement