Majeruhi wengine wanne ajali ya moto Morogoro wafariki, idadi yafikia 93

Friday August 16 2019

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Idadi ya vifo vya ajali ya lori la mafuta ya petroli lililoanguka kisha kuwaka moto eneo Msamvu mkoani Morogoro imeongezeka na kufikia 93 baada ya majeruhi wengine wanne kufariki leo Ijumaa Agosti 16,2019.

Vifo hivyo vinafanya idadi ya wagonjwa waliobaki kuwa 21 kati ya 46 waliokuwa wamefikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza baada ya kutembelea wagonjwa hao leo Ijumaa Agosti 16, 2019,  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu amesema madaktari wanafanya kila jitihada kuokoa maisha ya wagonjwa waliobaki.

Waziri Ummy amesema kila mgonjwa ana nesi wake anayemtazama kwa ukaribu.

Ameagiza kuanzishwa kwa kitengo maalum cha kuhudumia wagonjwa wanaotokana na ajali za moto kitakachokuwa na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Awali, Mkuu wa Idara ya Kitengo cha dharura cha MNH, Dk Juma Mfinanga amesema wagonjwa wanapewa huduma inayotakiwa na kwamba wote waliobaki wamewekwa ICU.

Advertisement

Amesema wagonjwa hao wamewekwa ICU ili kuongeza umakini wa juu zaidi katika kuwahudumia.

Advertisement