Makonda apigwa 'stop' kuingia Marekani

Muktasari:

  • Marekani imesema Makonda anashiriki kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wao.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amezuiwa kuingia nchini Marekani.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa Januari 31, 2020 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema mkuu huyo wa mkoa amezuiwa kuingia nchini humo pamoja na mkewe, Mary Massenge.

Inaeleza kuwa anazuiwa kutokana na tuhuma za  kushiriki kukandamiza haki za binadamu.

Inafafanua kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu alioufanya jijini Dar es Salaam ni pamoja na kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wao.

"Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda amehusika katika uvunjifu huo wa haki kupitia nafasi yake kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,” inasema taarifa hiyo.

SOMA ZAIDI

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo ametumia akaunti yake ya Twitter kutangaza zuio hilo.

Pia taarifa ya Wizara hiyo imeitaka Serikali ya Tanzania kuheshimu haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kujieleza na  haki ya mikutano ya amani.

Mwananchi limemtafuta Makonda jana usiku na leo asubuhi Februari Mosi, 2020 bila mafanikio na simu yake ya mkononi haikuwa hewani.