Makonda asema hawatazitaja hoteli wanapowekwa watu karantini kutokana na corona

Tuesday March 24 2020
makonda2 pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hawatazitaja hadharani hoteli ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuwahifadhi wageni kutoka nje ya nchi ambao wanatakiwa kuwekwa karantini kwa siku 14 kwa ajili ya uangalizi dhidi ya virusi vya corona.
Makonda ameyasema hayo katika ziara yake kukagua utekelezaji wa hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona, ambapo leo Jumanne Machi 24, 2020 ametembelea kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Tunafahamiana tabia zetu, ni kama vile ambavyo tungeambiwa Watanzania wote wakae ndani na uhakika kuna watu wangetoka nje kwenda kuchungulia nani ametoka, tungejikuta wote tupo mtaani, kwa hiyo kwasababu tunafahamiana tabia zetu tusingependa kuzitangaza zile hoteli,” amesema Makonda.
Aliongeza kuwa wageni wakifika uwanja wa ndege au kituo cha mabasi au bandarini, watapewa maelekezo ya maeneo yaliyotengwa na hoteli zilizotengwa ikiwemo gharama tofauti tofauti kadri kila mmoja anavyoweza kumudu.
Makonda amesema kuwa wakuu wa wilaya hivi sasa wapo kwenye vikao, kupanga na kuchagua hoteli hizo zilizotengwa kwa ajili ya huduma hiyo.
Vilevile, amewaagiza viongozi wa mitaa kushiriki kuwatambua wageni wanaoingia mitaani na wale watakaokuwa wamewekwa karantini kwa siku 14 ili kuhakikisha hawatoki hadi siku hizo zitimie.
Makonda pia amewaagiza viongozi wa mitaa kutotangaza hoteli zilizotengwa kwa ajili ya wageni hao kwa wananchi, ili kuepusha kuzua taharuki na pia kwa ajili ya usalama wa wageni hao.

Advertisement