Makonda asisitiza ukaguzi vyombo vya moto, akumbuka ajali ya Morogoro

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ametaka ukaguzi kwenye vyombo vya moto ufanyike kwa kina ili kuepusha ajali, huku akisisitiza bodaboda kuwaheshimu wanafunzi kwenye vivuko vya waenda kwa miguu

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataka wakazi wa jiji hilo wanaomiliki vyombo vya moto kuwa na utaratibu wa kukagua vyombo hivyo ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Amesema utaratibu wa kukagua magari unasaidia kubaini changamoto zilizopo na kuzifanyia marekebisho yanayoweza kuzuia ajali.

Makonda ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi walioshiriki shindano la michoro ya usalama barabarani lililoendeshwa na kampuni ya mafuta ya Puma Energy.

Amesema anaposikia ajali zimetokea mikoani huwa anamuomba Mungu kuepusha  ajali hizo zisitokee katika mkoa wa Dar es salaam.

“Huwa namuomba sana Mungu ajali zisitokee Dar, fikiria ajali ya Moro ingetokea huku watu wangapi wangepoteza maisha, mali ngapi zingeharibika, hasara kiasi gani ingepatikana,”

Makonda pia amewataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria na vivuko vya waenda kwa miguu kwani wamekuwa chanzo kikubwa cha ajali zinazoweza kuzuilika.

Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza kampuni ya Puma Energy kwa kuratibu mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa Shule za msingi na kueleza kuwa imesaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ajali kwa kundi hilo.

“Katika miaka sita ambayo Puma imetoa mafunzo haya kwa watoto tunaona vifo vinapungua, mwaka huu amefariki mtoto mmoja tu na wengine wanne kujeruhiwa.

“Takwimu hizi zinazoonyesha ni kiasi gani watoto wanaelewa matumizi sahihi ya barabara na niwaombe watu wazima hasa waendesha bodaboda muendelee kuwasaidia ili wawe salama,” amesema Makonda

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania Dominic Dhanah amesema kampuni yake inatambua umuhimu wa watoto na ndiyo maana imejikita katika kuhakikisha wanakuwa salama wanapokwenda shuleni na kurejea nyumbani.

“Tunafahamu watoto ni kundi ambalo lipo kwenye hatari ya kupata ajali wanapokwenda shuleni, tumeona tutoe mafunzo ya matumizi sahihi ya barabara na yamekuwa na matokeo chanya,”

“Mafunzo haya yanafanyika na huwa tunawashindanisha kupima uelewa wao kupitia sanaa ya uchoraji na leo hatimaye washindi wamepatikana kwa mkoa wa Dar es salaam,”

Katika shindano hilo mwanafunzi wa darasa la tano Emmanuel Masawe wa Shule msingi Kihamba aliibuka mshindi wa mchoro bora ambapo alipata kitita cha Sh500000.

Sambamba na zawadi hiyo Masawe ameiwezesha shule yake kupata zawadi  ya Sh4 milioni.