Mangula: Ukitaka udiwani, ubunge mapema tutakukata

Sunday February 16 2020

 

By Suzy Butondo, Mwananchi [email protected]

Shinyanga. Makamu mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula kwa mara nyingine amewaonya wanachama wa chama hicho tawala nchini Tanzania kutoanza mapema kampeni za kuwania udiwani na ubunge.

Amesema ni mwiko kwa kiongozi kutoa ahadi, zawadi, fedha, takrima au kushawishi kwa dini yake, akisisitiza kuwa watu wa namna hiyo wataenguliwa mapema kuwania nafasi hizo.

Mangula ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 16, 2020 katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwenye mkutano wake na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho mkoani Shinyanga.

"Tunaomba amani iwe kwa udiwani na ubunge, mkianza kukimbiakimbia na makundi ya watu 20 mtawavuruga wapigakura wenu kuweni na umoja na mshikamano, wakati  huu hutakiwi kutumia fedha zako kutafuta kura tutakuondoa,” amesema Mangula.

Siku tatu zilizopita akiwa katika ziara mkoani Shinyanga, Mangula alitamka kauli hiyo, akibainisha kuwa wale wote wanaosaka udiwani na ubunge kabla ya wakati wataondolewa mapema.

Kauli hiyo pia ilitolewa na makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 43 ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Advertisement

 

Advertisement