Mfumuko wa bei Septemba 2019 wapungua

Muktasari:

Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania (NBS) imesema kupungua kwa bei zisizo za vyakula kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 ikilinganishwa na bei ya Septemba mwaka 2018 ndio kumechangia kupungua kwa mfumuko wa bei mwaka unaoishia Septemba 2019.

Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania (NBS) imesema kupungua kwa bei zisizo za vyakula kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 ikilinganishwa na bei ya Septemba mwaka 2018 ndio kumechangia kupungua kwa mfumuko wa bei mwaka unaoishia Septemba 2019.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 8,  2019 kaimu mkurugenzi  wa sensa ya watu na takwimu za jamii wa NBS, Ruth Davison amesema mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 umepungua hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka unaoishia Agosti 2019.

" Hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Agosti 2019," amesema.

Amezitaja baadhi ya bidhaa zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 ni mafuta ya taa kwa asilimia 1.0, petroli (3.3), majiko ya gesi ( 1.5), dawa za kuulia wadudu nyumbani (2.2) na mafuta ya nywele (1.3).

Hata hivyo,Ruth  amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka unaoishia Agosti 2019.

Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, amesema Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 umepungua hadi asilimia 3.83 kutoka asilimia 5.00 kwa mwaka ulioishia Agosti 2019.

Amesema Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Septemba 2019 umepungua hadi asilimia

1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioishia Agosti 2019.