Mke, mume wavamiwa wakatwa mapanga wakiwa wamelala

Sunday December 15 2019

Umati wa watu waliofika kushuhudia tukio la

Umati wa watu waliofika kushuhudia tukio la wanandoa wawili kuvamiwa usiku wakiwa wamelala kisha  kukatwa mapanga na kuuwawa 

By Mary Clemence, Mwananchi [email protected]

Katavi. Hofu, simanzi na majonzi zimetawala kwa wakazi wa Mtaa wa Migazini  Manispaa ya Mpanda mkoa wa Katavi, baada ya wanandoa wawili kuvamiwa usiku wakiwa wamelala kisha  kukatwa mapanga na kuuwawa  na watu wasiojulikana.

Tukio hilo la kikatili, limetokea usiku wa kuamkia Desemba 15, 2019  nyumbani kwa wanandoa hao, Noel Muswanya (37) na mke wake aliyetambulika kwa jina moja la Siwema anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 27.
Mwananchi limefika eneo la tukio na kufanikiwa kuzungumza na mashuhuda, Everian Steven jirani wa marehemu amesema majira ya saa 7:30 usiku walisikia sauti ya kelele wakiomba msaada wakati wanashambuliana na wauaji hao.
“Tulitoka nje na mme wangu tukaona watu wamesimama nyumbani kwa marehemu, wakaturushia mawe, tukarudi ndani tukitaka kutoka wanarusha mawe kwenye nyumba yetu, muda mfupi kelele hazikusikika tena,” amesema.

Amesema waliamua kwenda nyumbani kwa wanandoa hao na kukuta nje kuna mtu amelala,  wakatoa taarifa kwa balozi na baadaye waligundua aliyekuwa nje  ni mke wa marehemu, alianguka wakati anakimbia kujiokoa na mmewe aliuawa akiwa ndani.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Ahamad Bahema amesema amepata taarifa hizo majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya kupigiwa simu na mjumbe wa eneo hilo.
“Tukio hili ni la kinyama na ni la kwanza kutokea licha ya kuwepo kwa matukio ya wizi yanayotokea mara kwa mara, nimeshuhudia na kutoa taarifa polisi,” amesema Bahema.
Shemeji wa marehemu, Edward Makanya amesema amepokea  taarifa hizo kwa masikitiko makubwa  saa moja kasorobo asubuhi.
“Dada nimemkuta nje na shemeji alikuwa sebleni,  nilikuwa namfahamu tangu utoto wake, nimekua naye, nimecheza naye nimeumia sana, namwachia Mungu,” amesema Makanya.

Polisi walifika eneo la  tukio na kuchukua miili ya marehemu ambayo imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Katavi.
Kamanda wa Polisi mkoani Katavi, Benjamini Kuzaga akizungumza na Mwananchi kwa simu, amesema yupo nje ya mkoa kikazi na hana taarifa hizo.
“ Mimi sipo Katavi na sina taarifa hizo,” amesema Kuzaga.

Advertisement