Mke wa DC Chemba amtetea mke mwenzake asipewe talaka

Monday August 19 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Medilina Mbuwuli, mke wa mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga ameiomba Mahakama ya Mwanzo  Ukonga kutovunja ndoa ya mumewe na Ruth Osoro waliyofunga bomani.

Medilina ambaye alifunga ndoa kanisani na mkuu huyo wa Wilaya, amesema  Odunga hana sababu rasmi za kuvunja ndoa hiyo.

Ameeleza hayo leo Jumatatu Agosti 19, 2019 katika mahakama hiyo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya madai ya talaka namba 180 ya 2019 iliyofunguliwa na Odunga dhidi ya Ruth.

Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo ya Mwanzo, Elia Mrema mwanamke huyo amesema ndoa ya mke mwenzake isivunjwe bali mahakama imuamuru Odunga atunze familia zake kwa sababu hana sababu rasmi za kuvunja ndoa.

Mbali na kesi dhidi ya Ruth,  Odunga alifungua kesi nyingine ya madai ya talaka  namba 181 ya 2019 mahakamani hapo dhidi ya Medilina ambayo leo Jumatatu ilishindwa kuendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu, Christina Luguru  kwa sababu mzee mmoja wa baraza  kati ya wawili wanaoshiriki kuisikiliza kesi hiyo kufiwa. Na imepangwa kuendelea kusikilizwa Agosti 27, 2019.

Akiendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo, Medilina amesema  mwaka 2013 alipata taarifa kutoka kwa msiri wake kuwa mumewe  alikuwa anataka kumuoa Ruth kwa ndoa ya bomani lakini kwa bahati mbaya kutokana na usiri uliokuwepo hakuweza kujua tarehe waliyofungwa.

Advertisement

Alidai  kwa mara ya kwanza alimuona Ruth alipokwenda dawati la jinsia na watoto kulalamikia matunzo yake  na  mtoto wake na Ruth alikwenda na Odunga kama mke aliyemsindikiza  mume.

“Lakini baada ya kupitia mateso mengi ya ndoa na kutelekezwa yeye na mtoto wake, Ruth alinitafuta akanipata  na kuomba nimsamehe kwa kuwa wakati anafunga ndoa Odunga alimdanganya kuwa hana mke, akasema anaomba msamaha tuishi kama ndugu na watoto wetu ni ndugu kaka na dada,” alieleza Medilina mahakamani hapo.

Amesema walizungumza mengi  kuhusu mume wao huyo  kwamba ni mtu wa kutanga tanga  katika majumba ya wanawake, mtu wa starehe, hashikiki  na hatoagi hata matunzo   ya watoto.

Akiendelea kutoa ushahidi mahakamani hapo, Medelina alieleza yeye na Ruth waliendelea kuishi kama ndugu na wamekuwa wakisaidiana  hadi walipofunguliwa kesi za madai ya talaka  na kwamba iwapo mahakama itahitaji cheti cha uthibitisho wa ndoa anacho.

Hakimu alisema nini, mke huyo alimzungumziaje zaidi mme wake na mengine mengi usikose gazeti lako la Mwananchi kesho Jumanne Agosti  20, 2019.

Advertisement