Msuya: Makatibu wakuu tulichanga fedha za ujenzi wa hospitali Pangani - VIDEO

Waziri mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amesema enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, watumishi wa umma walikuwa na moyo wa kuendeleza nchi na kuna wakati makatibu wakuu wa wizara walichanga fedha kujenga hospitali ya Wilaya ya Pangani, Tanga.

Msuya alisema hayo alipozungumza na gazeti hili kuhusu miaka 20 bila Mwalimu Nyerere ambaye alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza.

“Kitu kimoja ambacho nataka nikuambie ambacho sikioni siku hizi ni kwamba kwa wale waliochaguliwa walikuwa na moyo, morali wa kufanya kazi na kutafsiri sera za serikali kwa vitendo ili kukidhi matazamio ya wananchi,” alisema Msuya.

Msuya alisema moyo wa kuchapa kazi na kujitolea wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere ulikuwa kwa wote waliokuwa serikalini, mawaziri pamoja na makatibu wakuu.

Alisema pia Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa mchapakazi, alikuwa anafanya kazi kwa kusoma nyaraka zote za Serikali alizowasilishiwa zikiwamo za miradi mbalimbali na mifumo ya serikali kuileta kwenye kilimo.

“Sisi katika vikao vyetu tukasema lazima tufanye kazi, tusimwangushe Mwalimu, tuonyeshe Taifa letu na Mwalimu kwamba tunaweza kufanya kazi,” alisema Msuya.

Msuya ambaye amewahi kushika nafasi ya uwaziri mkuu mara mbili, wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere na wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema pia walifanya bidii kwenye kazi kuwaonyesha wakoloni kwamba wanaweza bila wao.

“Mfano wa moyo wa kujitolea ni kwamba wakati huo watumishi wa umma ambao ni wazawa tulisema tufanye kitu kimoja ambacho kitatuonyesha tunavyoleta msukumo wa taifa, kiongozi wetu alikuwa anaitwa Joseph Namata alikuwa katibu ofisi ya Rais.

“Tukaamua tuchange fedha kujenga Hospitali ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Na tulifanya vipo vitu vingi kutokana na moyo tuliokuwa nao tulifanya kwa ajili ya Taifa letu na kuwatia watu moyo,” alisema Msuya na kuongeza kwamba fedha hizo zilichanganywa na makatibu wakuu na ilikuwa kati ya mwaka 1961 au 1962.

Nyerere atishia kuvunja Bunge

Msuya alisema wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjika alikuwa waziri wa fedha na wakawa na jukumu la kuingiza kodi za jumuiya kwenye kodi za ndani.

Alisema walipeleka muswada wa sheria bungeni wa kuoanisha kodi na kubadili viwango ili kuziba pengo la yaliyokuwa mapato ya jumuiya. Hata hivyo, wabunge walikataa kupitisha mabadiliko hayo.

“Wabunge wakang’aka kwelikweli. Nafikiri walikuwa wanaona kwamba zile posho zao walizokuwa wanapata zitaondolewa. Tulikuwa na Mzee (Rashidi) Kawawa wakati ule ndiye aliyekuwa waziri mkuu.

“Tukahangaika hapo, ikashindikana tukamuomba Mwalimu aje azungumze nao, lakini akakataa na akasema waacheni waende na alitushauri tuahirishe Bunge, alisema.

“Wakati wabunge wanakwenda nyumbani, Mwalimu akaita Redio Tanzania, akasema wabunge wamerudi nyumbani kwa sababu wamekataa sheria tuliyotunga ya kutafsiri kwa vitendo hoja zetu za Azimio la Arusha, tumewapa nafasi wakashauriane na baada ya wiki mbili tutaitisha tena Bunge.

“Wakija hapa wakikataa nalivunja hili Bunge ili twende tukapigiwe kura na wananchi,” alisema Msuya akimnukuu Mwalimu Nyerere.

Alisema walipofika majimboni wananchi waliwauliza sababu za kukataa mambo ya misingi ya Azimio la Arusha. “Iliwapa shida sana, waliporudi tukaenda na muswada uleule wakakubali tukapitisha.”

Nyerere amtuma Benki ya Dunia

Msuya alitoa mfano wa changamoto za kimataifa kwamba kuna wakati Mwalimu Nyerere alimtuma kwenda Marekani kujadiliana na Benki ya Dunia kuhusiana na hali ya uchumi wa nchi.

Alisema kuna mambo ambayo walikuwa wamekubaliana na Benki ya Dunia lakini mpaka wakati Mwalimu Nyerere anastaafu walikuwa hawajayamaliza yote.

Wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa ameondoka madarakani, alimwambia Rais Ali Hassan Mwinyi kwamba, “nafikiri hawa watu watakupa nafuu kidogo, mimi wataniacha kwa vile wanafikiri nilikuwa na msimamo mkali.

“Nikatumwa (na Mwinyi) kumalizia yale mazungumzo na Benki ya Dunia na IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa), tukakubaliana kwamba kama haya yakikubalika na Serikali na yakawekwa kwenye bajeti ya fedha zitatoka.

“Kabla sijaenda kwenye huo mkutano wa Marekani, nilimuomba Rais anipe waziri mwingine twende naye, nikamchagua waziri Paul Bomani. Tuliporudi tulitoa taarifa kwenye baraza la mawaziri, wakasema sawa fanyeni,” alisema Msuya.

Alisema baada ya kikao cha baraza la mawaziri walianza kutayarisha bajeti wakizingatia makubaliano ya Benki ya Dunia na IMF.

“Baada ya siku mbili Rais akaitisha tena kikao cha Baraza la Mawaziri, akasema ‘hebu elezeni tena mambo mliokubaliana huko’. Tukaanza kuwa na wasiwasi kumetokea nini. Tukaeleza akawauliza mawaziri wakakubali tuendelee na utekelezaji.

“Siku ya tatu, ilikuwa ndio bajeti ni kesho, kwa kawaida bajeti ilikuwa inasomwa Alhamisi. Jumatano Rais akaitisha tena kikao cha baraza la mawaziri ‘akasema jamani hii kitu tutazame tena maana sipati usingizi. Basi tukafikiri sasa labda hana imani na sisi, imebaki siku moja bajeti.

“Tukamwambia Mzee tumebakisha kesho tunatakiwa tuwasilishe bajeti bungeni. Sasa kama hatutapata uamuzi wa mwisho itakuwa matatizo. Safari hii akaamua kumfanya kila waziri aseme.

“Kulikuwa na mawaziri watatu au wanne ambao hawakubaliana na sisi mmoja alikuwa msimamizi wa viwanda, usafirishaji na mawasiliano na mwingine alikuwa wa ideological (itikadi) tu hivi.

“Wakati huo kama fedha hazingekuja hizo huduma za usafiri na simu zingesimama, viwanda vingefanya kazi chini uwezo wake, kwa hiyo ingebidi hata fedha za kuendesha serikali labda mchapishe noti, badala ya kutengeneza kitu kama soda na bidhaa zingine ili mtoze kodi.

Msuya alisema baadaye waziri Kingunge Ngombale-Mwiru akatoa hoja kwamba fedha zinazotarajiwa kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa zitasaidia kukuza uchumi na vitu kuonekana madukani, kwani hali ilikuwa mbaya hata nyembe ilikuwa shida kupatikana dukani.

“Mimi nasema badala ya kusema tukatae, tukatae tunajidanganya maana tusipofanya uamuzi tunaweza kugeukiwa tu na watu wetu, wakasema hawa watu wameshindwa kutawala afadhali tukubali. Rais akauliza, jamani mnaonaje hilo wakasema haya. Tukapewa idhini tukaenda bungeni,” alisema Msuya.

Msuya alisema kutokana na baraza la mawaziri kuitishwa mara tatu kwa hoja ileile, aliamua kumfuata Rais Mwinyi kumuuliza kama alikuwa hana imani nao ili wajiuzulu.

“Nikamwambia tuliporudi kutoka Marekani tulileta cabinate paper ikakubaliwa, ukatuita karibu mara mbili ni nini, ulikuwa huna imani na sisi ili tujiuzulu au namna gani.

“Akasema hapana bwana, kilichokuwa kinanisumbua mkishaondoka kuna watu hapa wa University (Chuo Kikuu), wachumi wanasema ukifanya hivi utapinduliwa na hivi na hivi, lakini kitu cha ajabu kilichonishangaza nikawaambia basi kama hamtaki nifuate haya mapendekezo ya kina Msuya na Bomani hebu leteni ya kwenu ili tutatue mara moja, tatizo liko, leteni wazo na nyinyi maprofesa. Lakini wamekwenda hawajarudi,” alisema Msuya akimnukuu Mwinyi.

“Wanakuja hapa wanakudanganya hivi na hivi, lakini ikija kwenye vitendo hakuna,” alisema Msuya.