Mvua iliyotikisa Dar ilivyoacha misemo mitandaoni

Saturday October 17 2020
mvuapic

Dar es Salaam. Si ajabu kusikia maneno mbalimbali yakiibua mjadala katika mitandao ya kijamii kila linapotokea tukio kubwa nchini Tanzania.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo hutumia matukio husika kufanya masihara, na moja ya matukio hayo ni mvua kubwa iliyonyesha Oktoba 14 na 15, 2020 jijini Dar es Salaam na kusababisha madhara katika baadhi ya maeneo huku watu 12 wakiripotiwa kufariki dunia.

Mvua hizo zilisababisha barabara kadhaa katika Jiji la Dar es Salaam kufungwa huku foleni kubwa wakati wa jioni sambamba na usafiri kuwa wa shida vikisababisha  baadhi ya wananchi  kufika majumbani mwao usiku.

Hali hiyo iliibua misemo kadhaa huku wengine wakihusisha kuchelewa kurudi majumbani na mambo mbalimbali pamoja na kuwadhihaki wanaoishi mabondeni.

Miongoni mwa misemo iliyotawala mitandaoni ni ile inayolaumu madalali wa nyumba  na viwanja vilivyopo mabondeni, “madalali  wamezima simu, hawataki lawama leo.”

Kwa wale wenye magari nao waliwabeza wasio na magari waliposema, “mliojenga kabla hamjanunua gari leo pandeni nyumba zenu.”

Advertisement

Wapo waliosema, “bosi kutokana na nyumba yangu kujaa pamoja na barabara kufungwa sitoweza kufika ofisini.”

Mpaka inafika Alhamisi Oktoba 15, 2020  baadhi ya watu ilielezwa kuwa walikuwa hawajafika majumbani, “kuna mwamba bado yuko kwenye foleni?”

Kwa wanandoa nao hawakuachwa wapoe kwani nao walitengenezewa msemo wa masihara kama, “unasema umenimis, huu ujumbe wangu au?”

Wakati wakazi wengi wakichelewa kufika nyumbani siku ya Jumatano kutokana na foleni kubwa za magari barabarani, baadhi ya watu walitoa ushuhuda akiwemo Zainab Rajab ambaye ni mwandishi wa East Africa TV akisema,

“Kutokana na mvua ya jana, nimetoka ofisini maeneo ya Mwenge saa 11:00 jioni kuelekea kwangu Bungoni, lakini kufika barabarani  foleni ilikuwa haisogei na nimefika nyumbani saa 11 alfajiri ya leo,” aliandika Zainab kwenye ukurasa wa Twitter ya TV hiyo.  

Licha ya baadhi ya watu kubeza ujumbe huo, Mussa Cmb alijibu, “Kama Hupo Dar huwezi kuelewa na kuamini! ,Watu wa Mbezi walilazimika kupita Salander bridge au Ilala kwasababu Jangwani hapakuwa panapitika. Hii ilipelekea foleni kubwa mno na vilevile Kinondoni Mkwajuni palifungwa pia so just imagine (hebu fikiri).”

 

 

Advertisement