Mwanafunzi ajiua baada ya kudhalilishwa na mwalimu kwa kukosa taulo za kike

Muktasari:

Polisi nchini Kenya walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wazazi hao zaidi ya 200 waliokuwa wamepiga kambi nje ya shule.

Nairobi, Kenya. Mwanafunzi mmoja nchini Kenya amejiua baada ya kuzomewa darasani kutokana na sare yake kuchafuka na madoa ya damu alipokuwa kwenye hedhi.

Mama wa mwanafunzi huyo mwenye miaka 14 alidai kuwa binti yake alijinyonga baada ya kudhalilishwa na mwalimu.

Vyombo vya habari vya Kenya viliripoti kuwa tukio hilo lililotokea Ijumaa iliyopita lilisababisha ghasia kubwa kutoka kwa wazazi walioandamana kulaani kitendo hiko.

Polisi nchini Kenya walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wazazi hao zaidi ya 200 waliokuwa wamepiga kambi nje ya shule.

Mwaka 2017, Kenya ilipitisha Sheria ya kugawa taulo za kike bure mwaka 2017 kwa wanafunzi wa shuleni zote za umma.

Akizungumza na gazeti la Daily Nation la Kenya, mama wa binti huyo alidai mwalimu alimuita mwanafunzi huyo mchafu' na kumtaka atoke nje Shuleni ya Kabiangek iliyopo Magharibi mwa mji mkuu Nairobi.

''Hakuwa na pedi. Na damu ilipochafua nguo zake, aliambiwa atoke darasani na asimame nje,” mama huyo alinukuliwa na gazeti hilo..

Alieleza kuwa binti yake alirejea nyumbani na kumwambia mama yake kilichotokea shuleni, lakini alipokwenda kuchota maji alijinyonga.

Wazazi wake waliripoti tukio hilo polisi lakini imedaiwa hakukuwa na hatua zozote zilizochukuliwa.

Nation limeripoti.

Pamoja na wazazi wengine walikusanyika nje ya shule siku ya Jumanne. Polisi walifika na kuwakamata watu watano wakati waandamanaji walipofunga barabara na kuvunja geti la shule, ripoti zimeeleza.

Kamanda wa polisi jijini Nairobi, Alex Shikond alisema mazingira ya kifo cha binti huyo yanachunguzwa.

Hata hivyo, mkuu wa shule hiyo alikataa kuzungumzia tukio hilo.